KISHAPU YAPONGEZWA UTEKELEZAJI KWA VITENDO FALSAFA YA MWENGE WA UHURU

 
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda akizungumza alipokuwa wilayani Kishapu mkoani Shinyaga Agosti 18,2026

Na Sumai Salum-Kishapu

Mwenge wa Uhuru umehitimisha mbio zake Wilayani Kishapu mkoani Shinyanga kwa kukagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo, huku Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, akiupongeza Uongozi wa Wilaya, Halmashauri, wananchi na wadau kwa utekelezaji wa miradi yenye kugusa maisha ya wananchi.


Akizungumza wakati wa mbio hizo, Mwang’onda amesema utekelezaji wa miradi iliyotembelewa Kishapu unaonesha kwa vitendo namna falsafa ya Mwenge wa Uhuru inavyotekelezwa, ikiwemo kuimarisha huduma za kijamii, kuchochea shughuli za kiuchumi, kuibua fursa na kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika kujiletea maendeleo.


“Mwenge wa Uhuru umeridhishwa na utekelezaji wa miradi tuliyoitembelea Wilayani Kishapu. Tunawapongeza Serikali, viongozi, wananchi na wadau kwa ushirikiano wao. Miradi hii inaonesha kuwa rasilimali zinapotumika kwa uadilifu na kusimamiwa vizuri, zinaweza kubadilisha maisha ya wananchi,” amesema Mwang’onda.

Mkuu waWilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi (aliyebeba Mwenge wa Uhuru 2026) wakati akiingia kwenye viwanja vya makabidhianokwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Julius Mtatiro mara baada ya kumaliza mbio zake wilayani humo Agosti 19, 2026


Amesema pamoja na kukagua miradi, Mwenge wa Uhuru 2026 umeendelea kuhamasisha wananchi kulinda amani, umoja na mshikamano wa Taifa, akisisitiza kuwa amani ni msingi wa maendeleo na kila mwananchi ana wajibu wa kuilinda kwa kuepuka vitendo vinavyoweza kuvuruga utulivu wa nchi.


Aidha, amewataka wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali chini ya Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kuachana na matumizi ya nishati zinazochangia uharibifu wa mazingira na madhara ya kiafya, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza uelewa wa jamii kuhusu faida za nishati safi.

Katika Kijiji cha Songwa, Mwenge ulikagua na kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Serikali ya Kijiji unaogharimu Shilingi milioni 47, huku ukisisitiza umuhimu wa kuwa na mazingira bora ya utendaji wa Serikali ngazi ya kijiji kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.


Mwenge pia ulikabidhi trekta lenye thamani zaidi ya Milioni 50 kwa Kikundi cha Vijana Wachapakazi Songwa, lililopatikana kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri. Mwang’onda ameupongeza uongozi kwa kutumia fursa hiyo kuwawezesha vijana kiuchumi na kuwataka wanufaika kulitumia trekta hilo kwa tija ili kuongeza uzalishaji, ajira na kipato.


“Tunawapongeza Halmashauri kwa kutumia asilimia 10 ya mapato ya ndani kuwawezesha vijana. Vijana mliopata trekta hili, mlichukulie kama fursa ya kujikwamua kiuchumi. Litumieni kwa uaminifu na tija ili linufaike kundi lenu na vijana wengine wengi,” amesema.


Mwang’onda pia amesisitiza umuhimu wa kuibua, kuhamasisha na kuwawezesha vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalumu, akiwataka wananchi kutumia fursa zinazotolewa na Serikali kupitia mikopo na programu mbalimbali ili kujenga shughuli za uzalishaji na kuongeza kipato.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Fatma Mohamed (aliyebeba Mwenge wa Uhuru 2026) wakati wakienda kuukabidhi manisipaa ya Shinyanga baada ya kumaliza mbio zake wilayani humo Agosti 19, 2026


“Wananchi, hasa wanawake, vijana na makundi maalumu, msikae kusubiri ajira pekee. Jiungeni katika vikundi, tambueni fursa zilizopo na zitumieni. Serikali imeweka mazingira na fursa za kuwawezesha wananchi kiuchumi; ni wajibu wetu kuzitumia kwa ufanisi,” amesema.


Akizungumzia Mradi wa Ujenzi wa Shule ya Sekondari Masagala uliogharimu zaidi ya Shilingi milioni 282, Mwenge umepongeza Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu na kuwataka wananchi kutunza miundombinu hiyo ili iendelee kuwahudumia wanafunzi kwa muda mrefu.


Katika Kata ya Maganzo, Mwenge ulikagua Soko lenye thamani ya Shilingi milioni 280 pamoja na jengo lenye huduma za CRDB lililogharimu Shilingi milioni 700, huku ukieleza kuwa miradi hiyo ina nafasi kubwa katika kuchochea biashara, kuongeza ajira na kipato pamoja na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha.


Mwenge pia umekagua Daraja la Dugushilu lenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 117.7 pamoja na Zahanati ya Dugushilu iliyojengwa kwa zaidi ya Shilingi milioni 122.7, na kupongeza Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya usafirishaji na huduma za afya na Kukagua na kuzindua upanuzi wa Mradi wa maji ya Ziwa Viktoria  ulioko Kata ya Mwataga wenye thamani zaidi ya Milioni 250

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Emmanuel Johnson (aliyebeba Mwenge wa Uhuru 2026) wakati wakienda kuukabidhi manisipaa ya Shinyanga baada ya kumaliza mbio zake wilayani humo Agosti 19, 2026


Aidha, Mwenge umeendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki katika utunzaji wa mazingira, kulinda vyanzo vya maji, kutunza miundombinu ya maji safi na salama na kuhakikisha miradi inayotekelezwa inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.


Kwa ujumla, Mwenge wa Uhuru umeeleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi iliyotembelewa Kishapu na kupongeza Uongozi wa Wilaya ukiongozwa na Mkuu wa Wilaya, Mhe. Peter Masindi, pamoja na Halmashauri ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Emmanuel Johnson, kwa usimamizi wa miradi na jitihada za kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi.“Mwenge wa Uhuru unawapongeza wananchi wa Kishapu, viongozi na wadau wote. Tunataka kuona miradi hii ikitunzwa, ikitumika ipasavyo na ikileta matokeo chanya kwa wananchi. Maendeleo ni jukumu la pamoja; Serikali inaweka mazingira, lakini wananchi na wadau wana nafasi kubwa ya kuhakikisha fursa hizi zinatumika kujenga maisha bora,” amesema Wazo.


Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Peter Masindi, amekabidhi Mwenge wa Uhuru kwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Mhe. Julius Mtatiro, amesema kuwa Mwenge wa Uhuru umetekeleza mbio zake Kilomita 128.7 huku miradi yote ikiwa na thamani ya shilingi Bilioni 1.855.


Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026 zinaendelea kubeba ujumbe wa kuhamasisha wananchi kushiriki katika maendeleo, kulinda amani na mshikamano wa Taifa, kutumia nishati safi ya kupikia, kutunza mazingira, pamoja na kuibua na kuwawezesha wanawake, vijana na watu wa makundi maalumu kiuchumi.



























































































 

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post