
Na Mbuke Shilagi-Kagera
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera, Peter Mkenda, amewataka wananchi kuchukua tahadhari za kiafya ili kujikinga na ugonjwa wa Ebola, kufuatia taarifa za kuthibitishwa kwa ugonjwa huo nchini Kenya, ambapo kwa mujibu wa taarifa alizozitaja, watu saba wameathirika huku mmoja akiripotiwa kufariki dunia.
Akizungumza kuhusu hali hiyo ofisini kwake, Mkenda amesisitiza umuhimu wa wananchi kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya, akiwataka kuepuka kugusa mizoga ya wanyama na kujiepusha na kutoa huduma ya moja kwa moja kwa mtu mwenye dalili zinazoweza kuashiria maambukizi ya Ebola bila kufuata taratibu za kinga.
Aidha, amewahimiza wananchi kupunguza safari na mikusanyiko isiyo ya lazima, huku akisisitiza kuwa hatua za kujikinga zinapaswa kuanza mapema ili kupunguza hatari ya maambukizi.
Amesema wananchi wanapaswa kuwa makini wanapobaini dalili zinazotia shaka na kutoa taarifa kwa mamlaka za afya ili wahusika wapate ushauri na huduma stahiki kwa wakati.
Mkenda amehitimisha kwa kuwataka wananchi kushirikiana na wataalamu wa afya na kuzingatia maelekezo rasmi, akieleza kuwa tahadhari na uwajibikaji wa kila mmoja ni muhimu katika kulinda afya za jamii.


Post a Comment