Mafunzo ya usalama migodini kwa wachimbaji kutoka majimbo saba ya Mkoa wa Shinyanga yamehitimishwa Aprili 24, 2026 kwa wito wa kuendeleza uchimbaji wa madini kwa njia salama, endelevu na wenye tija kwa Taifa.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini Mkoa wa Shinyanga (SHIREMA) ambaye pia ni diwani wa Kata ya Maganzo Wilayani Kishapu Mhe. Hamza Tandiko amesisitiza kuwa elimu iliyotolewa ni msingi muhimu wa kulinda maisha ya wachimbaji, kuhifadhi mazingira na kuongeza uzalishaji wenye tija.
Akirejea maelekezo yaliyotolewa wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Aprili 23, 2026 na Mkurugenzi wa Huduma za Leseni wa Tume ya Madini, Mhandisi Aziza Swedi, viongozi hao wamewahimiza washiriki kuyatekeleza kwa vitendo maarifa waliyojifunza, ikiwemo usimamizi bora wa migodi, uzingatiaji wa sheria na kanuni, pamoja na matumizi salama ya kemikali.
“Uchimbaji wa madini kwa njia salama unawezekana mkoani Shinyanga. Tunachotakiwa ni nidhamu, ushirikiano na kuzingatia maelekezo ya kitaalamu tuliyoyapata,” amesema kiongozi huyo.
Aidha, wamewakumbusha wachimbaji kuwa usalama ni jukumu la kila mmoja, wakisisitiza kuwa ni muhimu kuhakikisha wachimbaji wanaingia migodini salama na kurejea nyumbani salama kila siku.
Kwa upande wao, washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru Serikali na wadau wa sekta ya madini kwa kuendelea kuwajengea uwezo, wakiahidi kuwa mabalozi wa usalama na uzingatiaji wa sheria katika maeneo yao ya kazi.
Kaulimbiu ya mafunzo hayo imeendelea kusisitiza dhamira ya pamoja “Uchimbaji wa madini kwa njia salama unawezekana mkoani Shinyanga".
Post a Comment