MRADI WA MAJI WA TSH. BILIONI 124 KUWANUFAISHA ZAIDI WA WANANCHI 700,000 GEITA, KIHONGOSI APONGEZA


ZAIDI ya wananchi  700,000 kutoka kata 19 katika Mkoa wa Geita wanatarijiwa kunufaika na  mradi  mkubwa wa maji unaogharimu zaidi ya TSH. bilioni 124 katika utekelezaji wake.

Mradi huo unatarajiwa kuanza kufanya kazi Septemba 30 mwaka huu na kuzalisha jumla ya kita milioni 45 za maji kwa siku.
Hayo yalibainishwa leo Aprili 16,2026 Mbele ya Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Kenani Kihongosi alipokagua utekelezaji wa mradi huo uliopo katika Kata ya Senga Geita Vijijini mkoani Geita.
Akizungumza  baada ya kukagua mradi huo Kihongosi amesema huo  ni miongoni mwa miradi ya maji 28  ambayo inatekelezwa nchi nzima na unatarajiwa kupeleka mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa upatikanaji wa maji safi na salama kwa ufanisi na kwa muda mrefu.
Amesema katika ilani ya Uchaguzi iliyopita, serikali iliahidi kuhakikisha huduma ya maji mijini inafikia asilimia 95 na vijijini asilimia 85, lakini mradi huo unapokamilika, watavuka lengo hilo na kufikia upatikanaji wa maji kwa asilimia 100. 
Amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa matanki makubwa matano ya kuhifadhia maji pamoja na mtandao wa mabomba wenye urefu wa kilomita 76, huku kilomita 71 tayari zimeshakamilika na zimebaki kilomita tano tu kukamilisha mtandao wote.
“Kwa kweli nikawa naona maajabu mengi, tumekagua miradi mingi, lakini huu ni mmoja wa miradi mikubwa sana. Hongereni sana, niwapongeze viongozi,  wataalamu na wasimamizi wa mradi  kwa weledi wao, mmeonesha  umiliki mkubwa wa kitaaluma na kuhakikisha kazi inafanyika kwa ufanisi,” amesema Kihongosi.
Awali, akisoma taarifa ya mradi huo Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (GEUWASA), Mhandisi Frank Changawa amesema  gharama ya mradi huo ni dola milioni 53.463, na hadi sasa utekelezaji umefikia asilimia 80 ya kazi nzima ya ujenzi na miundombinu.
Mradi huu unatarajiwa kuhudumia zaidi ya wakazi 700,000 kwa maji safi na salama na unatarajiwa kukamilika Septemba 30, 2026 chini ya Mkandarasi Afcons infrastructure Limited and Vijeta Projects and Infrastructure Limited.

 

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post