
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesisitiza wajibu wa kila mmoja kulinda amani, umoja na mshikamano wa Watanzania, akibainisha kuwa staha kwenye kazi haiwezekani bila ya amani na hakuna ustawi wa mfanyakazi bila ya amani na utulivu kwenye jamii.
"Kazi haiwezi kuwa na staha bila ya amani na hakuna ustawi wa Mfanyakazi bila utulivu wa Taifa, sasa ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa tofauti zetu hazigeuki kuwa sababu ya kuhatarisha misingi ya amani, umoja na mshikamano tulioachiwa na waasisi wetu. Tushikamane, tufanye kazi, tujenge Taifa letu na tujenge heshima ya nchi yetu." Amesema.
Rais Samia amebainisha hayo leo Ijumaa Mei Mosi, 2026 wakati wa kilele cha sherehe za wafanyakazi Kitaifa Mkoani Njombe, Maadhimisho yenye kuongozwa na kaulimbiu isemayo "Kazi zenye Staha ni Nguzo Imara kwa Maendeleo Endelevu Katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.
Katika hatua nyingine Rais Samia pia amesema Serikali imeanza rasmi kulipa malimbikizo mbalimbali ya wafanyakazi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi yake ya kuboresha mazingira ya kazi na kuhakikisha staha kwa watumishi wa umma na sekta binafsi.

Kwa mujibu wa Rais Samia, hatua hiyo ni uthibitisho wa dhamira ya serikali kuhakikisha haki za wafanyakazi zinalindwa na kutekelezwa kwa vitendo, sambamba na kuimarisha dhana ya kazi zenye staha kama inavyoelekezwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) na lengo namba 8 la maendeleo endelevu.
Amesema kuwa serikali inatambua mchango mkubwa wa wafanyakazi katika safari ya maendeleo ya taifa, na ndiyo sababu imeweka kipaumbele katika kutatua changamoto zinazowakabili, ikiwemo malimbikizo ambayo yamekuwa yakisababisha usumbufu kwa watumishi kwa miaka mingi.

Post a Comment