WANANCHI SHINYANGA KUNUFAIKA NA HUDUMA ZA KISHERIA BURE


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ,Mboni Mhita akizungumza na vyombo vya habari kuhusu kampeni ya Samia Legal Aid.


Na Mwandishi Wetu



Wananchi wa mkoa wa Shinyanga wanatarajiwa kunufaika na huduma za msaada wa kisheria bure kupitia kampeni ya kitaifa ya Samia Legal Aid, inayolenga kuwasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali za kisheria.


Kampeni hiyo itatekelezwa katika mkoa wa Shinyanga kuanzia Mei 6 hadi Mei 20, 2026, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali ya awamu ya sita kuhakikisha wananchi wanapata haki na huduma za kisheria kwa urahisi.


Akizungumza na vyombo vya habari Mei 5, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amesema timu ya watoa huduma za msaada wa kisheria itafika katika kata zote 130 za mkoa huo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.


Amesema kampeni hiyo ni awamu ya pili ya utekelezaji wake mkoani humo, ikilenga kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi wanaokumbana na migogoro na changamoto mbalimbali za kisheria, huku ikipunguza gharama ambazo wangetumia kufuata huduma hizo.


“Hii ni fursa muhimu kwa wananchi kwani huduma hizi zitawafikia moja kwa moja katika maeneo yao. Serikali imejipanga kuhakikisha wananchi wanapata haki zao bila vikwazo vya kifedha. Rais Samia Suluhu Hassan tayari amelipia gharama zote za kampeni hii inayotekelezwa nchi nzima,” amesema Mhita.


Katika awamu ya kwanza ya kampeni hiyo iliyofanyika mwaka 2023, jumla ya migogoro 578 ilishughulikiwa na kati yake migogoro 378 ilitatuliwa, huku zaidi ya wananchi 22,000 wakifikiwa na huduma hiyo.


Kwa mujibu wa Mhita, kampeni ya mwaka huu itaendeshwa kwa kipindi cha wiki mbili na itahusisha huduma mbalimbali zikiwemo ushauri wa kisheria, elimu kwa umma, uandaaji wa nyaraka za kisheria pamoja na uwakilishi katika vyombo vya mahakama.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kisheria Mkoa wa Shinyanga, John Shija, amesema wana matarajio makubwa katika awamu hii ya pili, akisisitiza kuwa kampeni hiyo itawafikia wananchi wa makundi yote na kusaidia kupunguza migogoro katika jamii.


Ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo muhimu ili kupata msaada wa kisheria na kutatua changamoto zinazowakabili kwa njia halali na endelevu.

PICHA ZA WANAHABARI MKOA WA SHINYANGA-HAPA CHINI



Afisa Maendeleo Mkoa wa Shinyanga,Rehema Edson
Mwenyekiti wa Msaada wa Kisheria Mkoa wa Shinyanga-John Shija.
Mkurugenzi Msaidizi wa uzingatiwaji wa huduma za msaada wa kisheria,Osborn Paiss wa Kampeni ya Samia legal Aid

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post