Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekabidhi vifaa tiba mbalimbali vyenye thamani ya Sh. Milioni 162 katika Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 ya TRA na utoaji wa Tuzo za Rais kwa Mlipakodi Bora zinazotarajiwa kutolewa Julai Mosi mwaka huu Mlimani City Jijini Dar es Salaam. Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo Hospitalini hapo Juni 28, 2026 Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema wameamua kurudisha kwa jamii mchango wa kodi ambazo wananchi wamechangia ili zisaidie kutoa huduma.
Amepongeza uwekezaji wa majengo uliopo Hospitalini hapo na kueleza kuwa ni matunda ya kodi ambayo yamewezesha maboresho hayo huku akisisitiza kuwa msaada wa vifaa hivyo ni hatua ya TRA kurejesha kwa jamii kutokana na kodi zinazokusanywa na baadae kurudi kwa watanzania kwa njia mbalimbali ikiwepo kuimarisha huduma za afya.
"Tumekuja leo kwa sababu mwezi wa saba TRA itatimiza miaka ya 30 ya kufanya kazi tuliyotumwa na watanzania ni miaka thelathini ya kuwashukuru wananchi ambao kwa kiasi kikubwa sana wamewezesha nchi yetu iwe na maendeleo", amesema.
Amesema TRA iliona njia mojawapo ya kuwashukuru watanzania ni kutoa kidogo kilichopo kwa jamii huku akitaja vifaa vilivyotolewa kuwa ni Vitanda vya wagonjwa 100, vitanda vya kujifungulia 10, Mashine ya Kusafishia damu kwa wagonjwa wa figo, Mashine ya kushtua Moyo na Mashine ya kusaidia kupumua.
Aidha Kamishna Mwenda amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa juhudi mbalimbali anazoendelea kuzichukua katika kuboresha mazingira ya afya nchini huku akiwataka wakuu wa taasisi mbalimbali kuhamasisha watu kuhamasisha watu walipe kodi kwa hiari
Amesema kwa kufanya hivyo huduma zinazotolewa na Hospitali zote nchini zitaimarika na hivyo kutoa matokeo chanya ikiwemo kulinda afya kwa watanzania wote siyo tu kwa wananchi wa Dar es Salaam.
Kwa upande wake Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa ya Mwananyamala Dkt. Aileen Balongo ameushukuru uongozi wa TRA kwa msaada huyo na kusisitiza kuwa utakwenda kusaidia utoaji wa huduma mbalimbali Hospitalini hapo.
Amesema Hospitali hiyo iliyoanzishwa Mwaka 1973, inahudumia wagonjwa 250 kila siku, Ina mahitaji mengi ya vifaa tiba kutokana na uwepo wa changamoto mbalimbali za kiafya zinazowakabili wananchi huku akisema msaada huo utasaidia kupunguza baadhi ya changamoto hizo.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt Mohammed Man'guna mbali na kuishukuru TRA kwa msaada huo pia amempongea Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa mabadiriko makubwa ambayo anaendelea kuyafanya katika sekta ya afya nchini huku akiwataka wananchi na watanzania kwa ujumla kuendelea kumuunga mkono.






إرسال تعليق