MJI WA KISERIKALI MTUMBA KUZINDULIWA NA RAIS SAMIA OKTOBA 30

Na Meleka Kulwa-Dodoma


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma Oktoba 30, 2026, mradi uliogharimu takribani Sh bilioni 700 na unaojumuisha majengo ya ofisi za wizara 26, taasisi 11 za Serikali na kilomita 59 za barabara za lami.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Oktoba 25, 2026, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema kuwa uzinduzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa hatua zilizochukuliwa na Serikali baada ya uamuzi wa kuhamia Dodoma.

Amebainisha kuwa mwaka 2016 Serikali ya Awamu ya Tano ilitangaza uamuzi wa kuhamia Dodoma kutoka Dar es Salaam, baada ya zoezi hilo kutofanyika kwa takribani miaka 43, na kwamba mchakato huo umefanyika kwa awamu.

Aidha, amebainisha kuwa katika awamu ya kwanza Serikali ilijenga majengo ya wizara katika Mji wa Serikali na baadaye kuhamia rasmi Dodoma.

Pia ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan iliendeleza jitihada zilizozalishwa na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwa kujenga majengo makubwa na ya kisasa ya Mji wa Serikali.

Huku akibainisha Kuwa ujenzi wa majengo hayo ulianza mwaka 2021 na umefanyika kwa ajili ya majengo ya wizara zote za Serikali, huku majengo hayo yakiwa yamezingatia mahitaji ya sasa na ya baadaye ya Serikali katika ngazi ya wizara na taasisi.

Aidha, amesema kuwa Mji wa Serikali una nafasi ya kutosha kwa ajili ya kuwahudumia Watanzania.

Uzinduzi huo uliokuwa ufanyike Septemba 8, 2026, uliahirishwa kufuatia kifo cha aliyekuwa mume wa Rais Samia, Bw. Hafidh Ameir Hassan, kilichotokea Septemba 7, 2026.


0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post