UBALOZI WA UHOLANZI WAMTANGAZA MELO WA JAMIIFORUMS KUWA MSHINDI TUZO YA HAKI ZA BINADAMU


Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Africa na mwanzilishi wa jukwaa la JamiiForums, Maxence Melo, ametangazwa mshindi wa Tuzo ya Haki za Binadamu ya Ubalozi wa Uholanzi ya mwaka 2026 (Netherlands Human Rights Embassy Tulip Award), kutokana na mchango wake katika kutetea uhuru wa kujieleza na haki za kidijitali nchini Tanzania.


Akitangaza mshindi huyo, Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Marjo Crompvoets, amesema Melo ametambuliwa kwa kazi yake kupitia JamiiForums katika kukuza mijadala ya umma na kulinda haki za watumiaji wa majukwaa ya kidijitali.


Pia ametambuliwa kwa mchango wake katika mageuzi ya sera, ikiwemo kuongoza muungano ulioshiriki kutetea kupitishwa kwa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi nchini Tanzania.


Tuzo hiyo hutolewa na balozi za Uholanzi katika nchi mbalimbali duniani kwa kutambua watu binafsi na taasisi zinazochangia kukuza na kulinda haki za binadamu.


Kupitia ushindi huo, Melo atapata kikombe cha shaba chenye umbo la ua la tulip, zawadi ya euro 5,000 pamoja na fursa za mafunzo, kujenga mtandao wa kimataifa na kutambuliwa kupitia vyombo vya habari.


Aidha, amechaguliwa kuwa miongoni mwa washindi watano duniani watakaotembelea Uholanzi.

EMBASSY TULIP AWARD 2026 – TANZANIA: MAXENCE MELO NAMED WINNER

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post