MSAADA WA KISHERIA WATAJWA KUWA SULUHISHO MIGOGORO YA ARDHI KISHAPU

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi akizungumza kwenye mkutano wa hadhara lengo likiwa ni utoaji elimu juu ya Kampeni ya Msaada wa kisheria ya Mama Samia Kijiji cha Lohumbo Kata ya Mwadui- Lohumbo Tarafa ya Mondo Mei 16, 2026

Na Sumai Salum- Kishapu


Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoa wa Shinyanga Mhe.Peter Masindi amesema Serikali imeendelea kuwathamini wananchi kwa kuhakikisha wanapata haki zao kupitia kampeni ya msaada wa kisheria  ya Mama Samia inayowafikia moja kwa moja katika maeneo yao, hatua ambayo imepokelewa kwa furaha kubwa na wananchi wa wilaya hiyo.


Akizungumza leo Mei 16, 2026 wakati wa mwendelezo wa kampeni ya msaada wa kisheria walipokuwa kwenye mkutano wa hadhara Kijiji cha Lohumbo Kata ya Mwadui- Lohumbo Tarafa ya Mondo, Mhe. Masindi amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alibaini kuwa wananchi wengi walikuwa wakipoteza haki zao kutokana na ukosefu wa elimu ya sheria huku wengine wakitumia gharama kubwa kufuatilia haki hizo bila mafanikio.


“Mhe. Rais alipata changamoto hizi kila anapopita ikiwa ni pamoja na njia ya mabango ambayo baadhi ya watu walikuwa wakiandika changamoto zao, hivyo mwaka 2023 akaanzisha programu hii yenye timu ya wataalamu wabobezi katika masuala mbalimbali ya migogoro ili wananchi waweze kupata msaada wa haraka na sahihi,” amesema Mhe. Masindi.


Amesema migogoro ya ardhi imekuwa chanzo cha migawanyiko katika familia, migogoro ya muda mrefu baina ya wananchi pamoja na vifo katika baadhi ya maeneo kutokana na watu wengi kutofahamu sheria na taratibu zinazohusu umiliki wa ardhi.


Aidha ameongeza kuwa kampeni hiyo imekuja wakati muafaka kwani wananchi wengi wa vijijini walikuwa hawana uwezo wa kuwafikia wataalamu wa sheria au kwenda mahakamani kutokana na changamoto za kifedha na umbali wa huduma hizo, hivyo amewataka wananchi kutumia jukwaa hilo kwa kujipatia elimu ya kina na kisha kuelewa namna ya kutatua migogoro mbalimbali waliyonayo.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Uzingatiaji wa Huduma za Msaada wa Kisheria, Osborn Paissi amesema kampeni hiyo inalenga kuongeza uelewa wa sheria kwa wananchi ili waweze kutambua haki zao na kuzitetea kwa kufuata taratibu sahihi za kisheria.


Amesema kupitia kampeni hiyo wananchi wanapata nafasi ya kusikilizwa changamoto zao moja kwa moja na wataalamu wa sheria, huku wakipewa ushauri wa namna ya kutatua migogoro yao kwa njia za amani bila kutumia nguvu au kuingia kwenye migogoro mikubwa zaidi.


Naye Diwani wa Kata ya Mwadui Lohumbo, Mhe. Francis Manyanda ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuwafikia wananchi kupitia kampeni hiyo akisema imeleta matumaini makubwa kwa wananchi wa Kishapu ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za migogoro ya ardhi hasa katika Kata hiyo.


Amesema elimu inayotolewa kupitia kampeni hiyo itasaidia wananchi kuelewa sheria za ardhi, kutambua mipaka yao halali pamoja na namna ya kufuata taratibu sahihi wanapopata migogoro.


Baadhi ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano huo, wamezungumza namna walivyofurahishwa na huduma hiyo wakisema imewasaidia kupata mwanga kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria ambayo awali yalikuwa yakiwasumbua.


Wananchi hao wamesema uwepo wa wataalamu wa sheria karibu na jamii utasaidia kupunguza migogoro isiyo ya lazima, kuimarisha amani katika familia na jamii pamoja na kuwapa wananchi ujasiri wa kudai haki zao kwa mujibu wa sheria.

" Tunampongeza Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu kwa jitihada anazozifanya kwa ajili ya wananchi kupata haki zao, hivyo tunatamani kuona watalamu wakija mara kwa mara ili kuleta msaada huu ambao umekuwa mkombozi kwetu" walisema Wananchi.
Mkurugenzi Msaidizi wa Uzingatiaji wa Huduma za Msaada wa Kisheria, Osborn Paissi akizungumza kwenye mkutano wa hadhara lengo likiwa ni utoaji elimu juu ya Kampeni ya Msaada wa kisheria ya Mama Samia Kijiji cha Lohumbo Kata ya Mwadui- Lohumbo Tarafa ya Mondo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Mei 16, 2026
Mwakilishi wa Katibu Tawala wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Tano Malale akizungumza kwenye mkutano wa hadhara lengo likiwa ni utoaji elimu juu ya Kampeni ya Msaada wa kisheria ya Mama Samia uliofanyika  Kijiji cha Lohumbo Kata ya Mwadui- Lohumbo Tarafa ya Mondo Mei 16, 2026
Diwani wa Kata ya Mwadui lohumbo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Francis Manyanda akizungumza kwenye mkutano wa hadhara lengo likiwa ni utoaji elimu juu ya Kampeni ya Msaada wa kisheria ya Mama Samia uliofanyika  Kijiji cha Lohumbo Kata ya Mwadui- Lohumbo Tarafa ya Mondo Mei 16, 2026
Mtendaji wa Kata ya Mwadui- lohumbo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Juma H. Juma
Mwenyekiti wa Kijiji cha Lohumbo Kata ya Mwadui Lohumo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Paul Elias Magida































































0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post