Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera Ismail Bukuku akizungumza na waandishi wa habari Septemba 16, 2026Na Mbuke Shilagi Kagera.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera imefanikiwa kusaidia Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kukusanya jumla ya Sh. 2,711,354,475.58 kutoka kwa makampuni binafsi yaliyokuwa hayajawasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza Septemba 16, 2026 katika ukumbi wa ofisi za TAKUKURU Manispaa ya Bukoba, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera, Ismail Bukuku, amesema jumla ya makampuni binafsi 146 yalifuatiliwa katika operesheni hiyo kutokana na kutowasilisha michango ya wafanyakazi wao kama inavyotakiwa.
Bukuku amesema operesheni hiyo ilifanyika kwa awamu mbili ndani ya siku 20, kwa lengo la kufuatilia fedha zilizopaswa kulipwa kama michango ya NSSF kutoka kwa makampuni hayo binafsi.
Amesema kupitia operesheni hiyo, NSSF imefanikiwa kukusanya Sh. 2,711,354,475.58, huku akieleza kuwa operesheni hiyo bado inaendelea kuhakikisha ulipaji wa michango yote unakamilika kwa asilimia 100.
Amesema kutowasilisha michango ya wafanyakazi kama inavyotakiwa ni kinyume na sheria za nchi, na kwamba ukwepaji wa michango hiyo kwa lengo la kujinufaisha ni kosa chini ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329.
Aidha, Bukuku ametoa wito kwa waajiri wengine ambao bado hawajakamilisha malipo ya michango au mafao ya waajiriwa wao kuhakikisha wanatimiza ahadi zao na kukamilisha malipo hayo.
TAKUKURU imesema itaendelea na ufuatiliaji huo hadi kuhakikisha michango yote inayodaiwa inakusanywa na kuwasilishwa NSSF kwa ukamilifu.

Post a Comment