KAMPENI YA MJUE JIRANI YAKO YATOLEWA KWA WATUMISHI WA HALMSHAURI YA KISHAPU


Kishapu


Ofisi ya Uhamiaji Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, imetoa elimu kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kuhusu masuala ya Uhamiaji, Uraia, Pasipoti na Hati za Safari, pamoja na umuhimu wa Kampeni ya Mjue Jirani Yako katika kuimarisha usalama wa Taifa.

Elimu hiyo imetolewa leo Septemba 15, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, ambapo Mkaguzi wa Uhamiaji, Robert Mahenge, amewaeleza watumishi kuhusu dhima ya Idara ya Uhamiaji, aina za uraia na ufafanuzi wake, pamoja na maana ya pasipoti na aina zake.

Katika mafunzo hayo, watumishi pia wamepewa ufafanuzi kuhusu taratibu za kuomba na kupata pasipoti, ikiwemo viambata vinavyohitajika wakati wa kuwasilisha maombi. Mahenge alitoa majibu na ufafanuzi wa maswali mbalimbali yaliyoulizwa na watumishi kuhusu huduma zinazotolewa na Idara ya Uhamiaji.

Aidha, watumishi wametakiwa kuwa wazalendo kwa kushiriki katika kulinda na kutetea rasilimali za Taifa, pamoja na kushirikiana na mamlaka na Ofisi za Uhamiaji kwa kutoa taarifa kuhusu uwepo wa wahamiaji wanaoingia au kukaa nchini bila kufuata taratibu, Sheria na Kanuni za nchi.

Mahenge amesisitiza umuhimu wa Kampeni ya Mjue Jirani Yako, akieleza kuwa ushiriki wa wananchi na watumishi katika kutoa taarifa sahihi kuhusu wahamiaji wasiofuata taratibu ni sehemu muhimu ya juhudi za kuimarisha usalama wa Taifa.

Kwa upande wake, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Afisa Tawala kutoka Ofisi ya Utumishi, Gabriel Pastory Kanoni, ametoa shukrani kwa Idara ya Uhamiaji kwa kufika katika Halmashauri hiyo na kutoa elimu ambayo amesema ni muhimu kwa watumishi katika kutambua na kutumia huduma zinazotolewa na Idara hiyo.

Kanoni amesema elimu hiyo imewasaidia watumishi kufahamu taratibu mbalimbali za kupata huduma za Uhamiaji, ikiwemo taratibu zinazohusiana na watumishi wapya wanaohitaji Vitambulisho vya Taifa na ambao hufika Ofisi ya Uhamiaji Wilaya ya Kishapu kwa ajili ya mahojiano kabla ya kuendelea na taratibu katika Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Amesema pia watumishi ambao wamepata wenza kutoka nje ya nchi wanapaswa kutumia fursa ya kupata elimu na huduma za vibali zinazotolewa na Idara ya Uhamiaji, huku akiwahimiza watumishi kutumia fursa za kusafiri nje ya nchi kwa kuzingatia taratibu halali, ikiwemo kutumia mfumo wa mtandao katika kuwasilisha maombi ya pasipoti.

Kanoni amehitimisha kwa kuahidi kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu itaendelea kushirikiana na Idara ya Uhamiaji na mamlaka nyingine za Serikali katika kuhakikisha taratibu za Uhamiaji zinafuatwa na kuchangia katika kulinda amani na usalama wa Taifa.







0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post