WANANCHI BUNAMBIYU WAWASILISHA KERO KWA DC MASINDI, ASIKILIZA NA KUZITATUA

MKUU wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Peter Masindi, amefanya mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Bunambiyu,Viitongoji vya Mwachanje Magu na Mwachanje Mhuge, kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Katika mkutano huo uliofanyika Septemba 25,2026, wananchi waliwasilisha kero ikiwemo upatikanaji wa maji, ubovu wa barabara pamoja na kukosa umeme, ambapo Mhe. Masindi amezisikiliza na kutoa maelekezo kwa watendaji wa Serikali kuzifanyia kazi.


Kuhusu tatizo la maji, wananchi wamesema wanalazimika kutembea umbali wa takribani kilomita 10 kufuata huduma hiyo. Kufuatia kero hiyo, Mkuu wa Wilaya amemtafuta kwa njia ya simu Mhandisi wa Maji wilayani humo na kumuelekeza kwenda eneo hilo kufanya ukaguzi na kuwasilisha taarifa kwake ifikapo ijumaa ya juma lijalo ili hatua zaidi zichukuliwe.


Kero nyingine ilikuwa miundombinu ya elimu ambapo wananchi wameeleza kuwa wameanzisha Shule shikizi ambayo tayari jengo lake limefikia hatua ya boma lakini bado halijamaliziwa. Mkuu wa Wilaya amewashauri Mwenyekiti wa Kijiji kukaa na Serikali ya Kijiji kujadili namna ya kupata suluhisho la kupaua jengo hilo wakati serikali ikiendelea na mikakati mingine ya uboreshaji miundombinu ya elimu kwenye vitongoji hivyo, na wananchi waliotenga eneo hilo kwa ajili ya shule wakihimizwa kuendelea kushirikiana kusimamia ili eneo hilo litumike kwa madhumuni yaliyokusudiwa.


Aidha, kuhusu barabara ya urefu wa kilomita 12, Mhandisi ameleza kuwa ombi hilo amelichukua na kulifikisha ofisini kwa ajili ya kufanyiwa kazi na hatua stahiki kuchukuliwa.


Katika suala la umeme, wananchi wameeleza kuwa Kitongoji chao bado hakijafikiwa na huduma hiyo. Kwa upande wake, TANESCO imeeleza kuwa iwapo REA itaanza utekelezaji wa mradi wa usambazaji umeme katika msimu huu, itahakikisha maeneo yenye uhitaji kama hayo yanazingatiwa.


Mhe. Masindi pia amewahimiza wananchi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kusomesha watoto wao na kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza kutokana na hali ya hewa, ikiwemo El Niño, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto zinazowakabili.

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم