BoT: FEDHA NYINGI MITAANI CHANZO CHA KUPANDISHA BEI YA BIDHAA

Meneja Uchumi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Jijini Mwanza, Issa Pagali, akizungumza kwenye kongamano lililoandaliwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tanzania (MISA-TAN), likiwakutanisha wadau kutoka taasisi za umma na binafsi kujadili namna ya kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi katika ukumbi wa BoT Jijini humo Oktoba 12,2026
Mwenyekiti wa MISA-TAN, Edwin Soko akizungumza kwenye kongamano la MISA TAN na Taasisi za umma na binafsi kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi Kisekta kupitia Uandishi wa Habari lililoanza leo Oktoba 12 na kumalizika Oktoba 13,2026 katika ukumbi wa mikutano Benki kuu ya Tanzania Jijini Mwanza 

Na Sumai Salum-Mwanza

Meneja Uchumi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mwanza, Issa Pagali, amesema uchapishaji wa fedha nyingi unaweza kuchochea mfumuko wa bei na kushuka kwa thamani ya fedha iwapo kiasi cha fedha kinachozunguka katika jamii kitaongezeka kwa kasi kuliko upatikanaji wa bidhaa na huduma sokoni.


Pagali ameeleza kuwa ongezeko la fedha katika mzunguko linaweza kuongeza matumizi na mahitaji ya bidhaa na huduma. Hata hivyo, mahitaji yanapokuwa makubwa kuliko uwezo wa uzalishaji na upatikanaji wa bidhaa, bei hupanda na kusababisha mfumuko wa bei, hali inayopunguza uwezo wa wananchi kununua bidhaa na huduma kwa kipato kilekile.


Ametoa ufafanuzi huo Oktoba 12, 2026, wakati wa kongamano lililoandaliwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tanzania (MISA-TAN), lililowakutanisha wadau kutoka taasisi za umma na binafsi kujadili namna ya kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi.


“Benki Kuu ya Tanzania huchapisha fedha kutokana na mahitaji muhimu yaliyopo. Benki ikichapisha fedha nyingi, husababisha matumizi makubwa ya fedha kununua bidhaa na kuongeza mahitaji yake, jambo linaloweza kupelekea mfumuko wa bei. Pia, benki ikichapisha fedha kwa wingi, thamani ya fedha hushuka,” amesema Pagali.


Kwa upande wake, Meneja Msaidizi wa BoT Mwanza, Stanley Nderingo, amesema hadi Juni 2026, benki hiyo ilikuwa imenunua tani 35 za dhahabu kwa lengo la kuimarisha akiba ya fedha za kigeni. Amesema kati ya kiasi hicho, tani tano zilikuwa zimeuzwa na zoezi la uuzaji likiendelea.


“Katika tani 35 za dhahabu ambazo benki imenunua, tayari tumeuza tani tano na bado tunaendelea,” amesema Nderingo.


Naye Mwenyekiti wa MISA-TAN, Edwini Soko, amewataka waandishi wa habari kuzingatia weledi, kuelewa majukumu yao na kuboresha ubora wa taarifa wanazoziandaa. Pia amezitaka taasisi za umma na binafsi kuimarisha ushirikiano na waandishi wa habari kwa kutoa taarifa na ufafanuzi kwa wakati wanapohitajika.


“Tunakutana na changamoto ya kutokupata taarifa kwa wakati pale tunapozihitaji. Niwaombe taasisi binafsi na za umma kuwa na ushirikiano na waandishi kwa kutoa taarifa na ufafanuzi kwa wakati pale ambapo mwandishi anapokuwa na uhitaji,” amesema Soko.

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post