DC MASINDI AINGILIA KATI MGOGORO WA MAJI IKONONGO, CBWSO YA MWIGIKO KUDAIWA MILIONI 2.8


Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Peter Masindi, ameingilia kati mgogoro wa malipo ya huduma ya maji kati ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama-Shinyanga (KASHWASA) na CBWSO ya Mwigiko, uliosababisha wananchi wa Kijiji cha Ikonongo, Kata ya Maganzo, kukosa huduma ya maji.


Mhe. Masindi amechukua hatua hiyo leo Jumatatu, Oktoba 26, 2026, katika kikao cha kutafuta suluhisho la mgogoro huo uliotokana na kutowasilishwa kwa wakati kwa malipo ya maji kutoka kwa  CBWSO ya Mwigiko kwenda KASHWASA, hali iliyosababisha athari kwa wananchi wanaotegemea huduma hiyo.


Katika kikao hicho, imeelezwa kuwa CBWSO ya Mwigiko inadaiwa jumla ya Sh milioni 2.8 na imekubali kulipa deni hilo ndani ya kipindi cha miezi minne. Aidha, Mhe. Masindi amesisitiza umuhimu wa wahusika kutekeleza makubaliano hayo na kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa wananchi bila usumbufu unaotokana na changamoto za malipo.


Mhe. Masindi ameelekeza wananchi wenye madeni ya maji kulipa ifikapo Ijumaa, Oktoba 30, 2026, huku CBWSO ya Mwigiko ikitakiwa kuimarisha ukusanyaji wa fedha na kuziwasilisha KASHWASA kwa wakati. Hatua hiyo inalenga kuzuia changamoto kama hiyo kujirudia na kuhakikisha wananchi hawaendelei kuathirika kutokana na madeni ya huduma ya maji.


Katika hatua nyingine, Mhe. Masindi amelitaka Jeshi la Sungusungu kushirikiana na wananchi kulinda miundombinu ya maji dhidi ya uharibifu, akisisitiza kuwa ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha miundombinu hiyo inalindwa ili huduma iendelee kupatikana kwa manufaa ya jamii.


Amesisitiza kuwa KASHWASA na CBWSO ya Mwigiko zinapaswa kuimarisha ushirikiano na kuweka utaratibu madhubuti wa ukusanyaji na uwasilishaji wa fedha za maji kwa wakati, ili changamoto za malipo zisijirudie na wananchi wa Ikonongo waendelee kupata huduma hiyo muhimu bila usumbufu.


Kwa upande wake, Meneja huduma kwa wateja John Zengo, ambaye ni Mratibu wa CBWSO kutoka KASHWASA, amesisitiza umuhimu wa kutekeleza makubaliano ya malipo ili kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi.


Diwani wa Kata ya Maganzo, Mhe. Hamza Tandiko, amesema wananchi wanahitaji huduma ya maji iliyo ya uhakika na wamekuwa wakitamani kufungiwa mita za malipo ya kabla LUKU/ Prepaid meter


katika vituo vyao vya maji. Amesema mfumo huo unaweza kurahisisha malipo kulingana na matumizi na kupunguza migogoro inayotokana na ukusanyaji wa fedha, hivyo ameiomba mamlaka husika kuangalia uwezekano wa kuutekeleza.


Tandiko, amewataka wananchi wote wenye madeni ya huduma ya maji kuhakikisha wanalipa madeni yao kwa wakati ili kusaidia kuimarisha upatikanaji wa huduma hiyo na kuepusha changamoto zinazoweza kusababisha maji kukosekana tena.





0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post