Kamishna wa Skauti Mkoa wa Shinyanga, ALT. Mussa M. Chama akizungumza wkati akiongoza kikoa cha Kamati Tendaji ya Skauti mkoani humo kilichofanyika Oktoba 9, 2026, katika ukumbi wa TARURA Mkoa
Na Sumai salum- Shinyanga
Kamati Tendaji ya Skauti Mkoa wa Shinyanga imefanya kikao chake Oktoba 9, 2026, katika ukumbi wa TARURA Mkoa wa Shinyanga, kujadili masuala mbalimbali yanayolenga kuimarisha shughuli za skauti, ikiwemo utambuzi na ufuatiliaji wa viongozi, tathmini ya maendeleo ya skauti mkoani humo na mafunzo ya skauti.
Kikao hicho kimeongozwa na Kamishna wa Skauti Mkoa wa Shinyanga, ALT. Mussa M. Chama, ambaye amewahimiza wajumbe kushirikiana, kuwajibika na kuweka mikakati ya kuimarisha ushiriki wa vijana katika shughuli za skauti, pamoja na kuhakikisha maazimio ya vikao yanatekelezwa.
Aidha Uongozi umeeleza namna ulivyowachukulia hatua za kinidhamu dhidi ya viongozi wanaoonekana kuwa wazembe katika kutekeleza majukumu yao, kwa lengo la kuimarisha nidhamu, uwajibikaji na ufanisi wa utendaji., sambamba na hayo imeelezwa kuwa Mkutano Mkuu wa Skauti Mkoa wa Shinyanga unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu, wenye lengo la kufanya uchaguzi wa viongozi wa Skauti wa Mkoa.
Katika majadiliano hayo, wajumbe wamesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano, kuwajengea uwezo viongozi na kuongeza uhamasishaji wa vijana kujiunga na skauti kupitia shule na jamii, ili kukuza maadili, uzalendo na uongozi bora, wamejadili masuala ya uongozi, tathmini ya maendeleo ya skauti, mafunzo na mikakati ya kuongeza ufanisi wa shughuli za skauti na umuhimu wa kuimarisha ushirikiano.
Aidha, kamati hiyo ilimtembelea Mjumbe wa Bodi ya Skauti Mkoa wa Shinyanga, ambaye pia ni Afisa Elimu Taaluma katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, George Ogutu, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kubadilishana mawazo kuhusu namna ya kuendeleza shughuli za skauti mkoani humo.
Kwa upande wake, Ogutu amesisitiza umuhimu wa skauti katika kuwajenga vijana kuwa na nidhamu, uzalendo, uongozi bora na uwezo wa kujitegemea. Alihimiza viongozi wa skauti kushirikiana na taasisi za elimu, walimu na wazazi ili kuwahamasisha vijana kujiunga na skauti na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya jamii.
"Kubwa zaidi nikupongeze Kamishina kwa umairi uliouonesha wa kuzingatia lika zote katika Kamati yako tendaji hasa Wanawake, Vijana na Wazee na wakiwa wanatokea si tu Wilaya moja bali kila wilaya za Mkoa huu hongera, zaidi sana mtambue tu mpo kwenye nafasi hizo kwa lengo la kulisaidia taifa katika mapambano mbalimbali" Ameongeza Mwl. Ogutu
Kikao hicho ni sehemu ya juhudi za Kamati Tendaji ya Skauti Mkoa wa Shinyanga katika kutathmini utekelezaji wa majukumu yake na kuweka mikakati ya kuimarisha skauti, huku ikilenga kukuza maadili, uwajibikaji na uongozi miongoni mwa vijana.
Mjumbe wa Bodi ya Skauti Mkoa wa Shinyanga, ambaye pia ni Afisa Elimu Taaluma katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, George Ogutu akizungumza na Kamati tendaji wakati walipomembelea Ofisini kwake kabla ya kuanza kikao chao mnamo Oktoba 9,2026 katika Ukumbi wa mikutano wa TARURA mkoani humo
Post a Comment