KINGA NA UCHUNGUZI WA MAPEMA KIPAUMBELE KATIKA KUDHIBITI MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA


Na Shaban Juma, WAF – Dodoma


Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuimarisha mikakati ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza nchini kwa kuongeza elimu ya afya, uchunguzi wa mapema na upatikanaji wa matibabu.


Amesema hayo leo, Oktoba 16, 2026, jijini Dodoma, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, wakati akiwasilisha taarifa ya Serikali kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kukabiliana na Magonjwa Yasiyoambukiza kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI.


Dkt. Samizi amesema magonjwa yasiyoambukiza, yakiwemo shinikizo la juu la damu, kisukari, saratani, magonjwa ya moyo, magonjwa sugu ya mfumo wa upumuaji na sikoseli, yanaendelea kuwa changamoto kwa afya ya wananchi na maendeleo ya Taifa, hivyo kuhitaji ushirikiano katika kuimarisha kinga, utambuzi wa mapema na matibabu.


Amesema takwimu za mwaka 2025/2026 zinaonesha kuwa jumla ya visa 6,166,692 vya wagonjwa wenye magonjwa yasiyoambukiza vilihudumiwa katika vituo vya afya nchini, ambapo visa 2,072,517 vilihusu shinikizo la juu la damu na visa 971,816 vilihusu kisukari. Aidha, wagonjwa 60,610 wa saratani na 116,634 wa sikoseli walipatiwa huduma katika kipindi hicho.


Katika kuimarisha kinga, Serikali inaendelea kutekeleza kampeni ya “Zijue Namba Zako”, iliyozinduliwa Mei 4, 2026, jijini Mwanza, inayolenga kuhamasisha wananchi kupima afya zao mara kwa mara. Hadi Septemba 2026, kampeni hiyo ilikuwa imewawezesha wananchi 17,388 katika mikoa 10 kupata huduma za uchunguzi wa afya ili kubaini mapema vihatarishi vya magonjwa yasiyoambukiza.


Aidha, Serikali imewajengea uwezo watumishi wa afya 2,890 kutoka vituo vya afya vya umma 711 katika halmashauri 184 ili kuimarisha huduma za uchunguzi na matibabu.


Vilevile, huduma za kibingwa zinaendelea kupanuliwa, ambapo hadi Septemba 2026 watoto 30 walikuwa wamepatiwa huduma ya upandikizaji wa uloto kwa ajili ya matibabu ya sikoseli katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.


Amesema changamoto zinazoendelea kukabili mapambano hayo ni pamoja na uelewa mdogo wa jamii kuhusu vihatarishi vya magonjwa, gharama za matibabu, upungufu wa wataalamu wa kibingwa na mtindo wa maisha usiofaa.












0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post