Na Sumai Salum-Kishapu
Wazee wilayani Kishapu mkoani Shinyanga wamepongeza juhudi za Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kwa kuwajali na kuwawezesha kupata huduma za afya na matibabu bure katika maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika kiwilaya hospitali ya Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Oktoba 1, 2026.
Wakizungumza wakati wa maadhimisho hayo, wazee hao wamesema huduma hiyo imewasaidia kupata matibabu na ushauri wa afya bila gharama, huku wakisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwepo kwa huduma endelevu zinazozingatia mahitaji na changamoto zinazowakabili wazee.
Mmoja wa wazee hao, Edward Sengeka, mkazi wa Isoso wilayani Kishapu, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuwajali wazee na kuwapatia fursa ya kupata huduma za afya, akisema hatua hiyo inaonesha kutambua mchango wao katika jamii.
Kwa upande wake, Elizabeth John, mwenye umri wa miaka 70, mkazi wa Kijiji cha Lubaga, ameishukuru Serikali kwa huduma hiyo na kuwataka wazee wenzake kutumia fursa zinazotolewa na Serikali, hususan huduma za afya, ili kuendelea kuishi maisha yenye afya na ustawi.
Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mwajuma Abeid akitoa elimu kuhusu siku ya wazee duniani kiwilaya yaliyofanyika kwa kutoa huduma za matibabu bure Oktoba 1,2026
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Shoma Sitta, amewahimiza wazee na jamii kwa ujumla kutambua aina mbalimbali za ukatili dhidi ya wazee, ikiwemo kupigwa, kutukanwa, kunyimwa mahitaji muhimu, kutelekezwa na kunyimwa haki zao.
Sitta amesema wazee wanaokabiliwa na ukatili au wanaoshuhudia vitendo hivyo wanapaswa kutoa taarifa kwa viongozi wa Serikali za mitaa, Maafisa Ustawi wa Jamii, Jeshi la Polisi au mamlaka nyingine zinazohusika, ili hatua stahiki zichukuliwe.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya wilaya hiyo, Mwajuma Abeid amesema Siku ya Wazee Duniani ni muhimu kwa kuwa inatoa nafasi ya kutambua mchango wa wazee katika jamii, pamoja na kutafakari namna ya kuboresha huduma na mazingira ya kuwawezesha kuishi kwa heshima na usalama.
Amesema Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wazee wanapata huduma muhimu, ikiwemo afya, ushauri na msaada wa kijamii, huku akiwataka wananchi kuendelea kuwaheshimu, kuwasikiliza na kuwasaidia wazee katika maeneo yao.
Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani mwaka 2026 yamebeba kaulimbiu “Zama za maisha marefu, tuboreshe huduma kwa wazee wetu” , inayosisitiza umuhimu wa jamii na Serikali kuendelea kuboresha huduma kwa wazee kadiri idadi ya watu wanaofikia umri mkubwa inavyoongezeka.
Kwa ujumla, maadhimisho hayo yamekuwa sehemu muhimu ya kuwakumbusha wananchi kuwa wazee ni sehemu ya msingi ya jamii na wanahitaji kuthaminiwa, kulindwa na kuhudumiwa kwa heshima. Ushirikiano kati ya Serikali, familia na jamii kwa ujumla ni muhimu katika kuhakikisha wazee wanaishi maisha yenye afya, amani, usalama na heshima wanayostahili.
Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Shoma Sitta akitoa elimu ya ukatili kwa wazee waliohudhuria maadhimisho ya siku ya wazee duniani kiwilaya yaliyofanyika kwa kutoa huduma za matibabu bure Oktoba 1,2026
Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Kelvin Mwandwanga akiendelea kuandikisha wazee hao ikiwa ni sehemu ya maadhimisho y Siku ya Wazee duniani kiwilaya yaliyofanyik kwa kutoa huduma za matibabu bure kwa wazee Oktoba 1, 2026
Mkazi wa Isoso wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Edward Sengeka alizungumza
Mkazi wa Isagara wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Kwimba John
Post a Comment