MSIMU UJAO 2026/27 BODI YA PAMBA KUNUNUA KWA USHINDANI



Na Mwandishi wetu, Mwanza.


BODI ya Pamba Tanzania (TCB) imeweka mikakati ya kuimarisha ushindani katika ununuzi wa pamba msimu wa 2026/2027, sambamba na kuimarisha uwazi kupitia mifumo ya kidijitali katika usambazaji wa pembejeo na matumizi ya mizani janja ili kulinda maslahi ya wakulima.

Akizungumza na vyombo vya habari, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania, Mhandisi Godwin Makori, amesema katika msimu huo hakutakuwa na mnunuzi mmoja pekee katika kituo cha ununuzi wa pamba, hatua inayolenga kuongeza ushindani na kuwapa wakulima fursa ya kupata bei nzuri ya zao hilo.

Amesema mfumo huo unatarajiwa kuwapa wanunuzi fursa ya kushindana, huku wakulima wakinufaika na uwezekano wa kupata bei inayolingana na thamani ya mazao yao.

Hatua hiyo inalenga kuongeza kipato cha wakulima na kuimarisha uchumi wa kaya zinazotegemea kilimo cha pamba.

Katika hatua nyingine, TCB inatarajia kusambaza tani 15,000 za mbegu za pamba katika wilaya 56 zinazolima zao hilo nchini katika msimu wa 2026/2027.


Hadi wakati wa maelezo hayo, tani 12,000 za mbegu zilikuwa tayari zimesambazwa katika maeneo mbalimbali Nchini.


Mhandisi Makori amesema matumizi ya mifumo ya kidijitali katika usambazaji wa mbegu na pembejeo nyingine yataongeza uwazi na uwajibikaji kwa kuwezesha ufuatiliaji wa pembejeo kuanzia zinapotolewa hadi zinapowafikia wakulima waliokusudiwa.

Mfumo huo pia unalenga kuboresha usimamizi wa usambazaji na kupunguza uwezekano wa kutokea kwa dosari katika zoezi hilo.

Ameeleza kuwa wakulima wanapaswa kusajiliwa kupitia Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) ili kurahisisha utambuzi wa walengwa na ufuatiliaji wa pembejeo wanazopokea.

Aidha, vituo vya ugawaji vitakuwa na kamati za kupokea mbegu, maafisa ugavi na wasimamizi watakaohakikisha zoezi hilo linafanyika kwa utaratibu unaostahili.

Kwa mujibu wa Mhandisi Makori, hatua hizo ni sehemu ya jitihada za kukabiliana na changamoto katika mnyororo wa thamani wa zao la pamba, ikiwemo ongezeko la gharama za pembejeo katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.
Kupitia mifumo hiyo, Bodi inalenga kuimarisha udhibiti na ufuatiliaji wa pembejeo ili kuhakikisha zinawafikia wakulima kwa ufanisi zaidi.

Kuhusu ulinzi wa wakulima wakati wa mauzo, amesema Bodi inaweka mikakati ya kutumia mizani janja katika vituo vya ununuzi wa pamba ili kuboresha usahihi wa vipimo na kupunguza uwezekano wa wakulima kupunjwa uzito wa mazao yao.

Mikakati hiyo inalenga kuboresha mnyororo mzima wa thamani ya pamba, kuanzia usambazaji wa pembejeo hadi ununuzi wa mazao, kwa kuimarisha uwazi, kuongeza tija na kulinda maslahi ya wakulima.

Utekelezaji madhubuti wa mikakati hiyo unatarajiwa kuboresha mazingira ya biashara ya pamba nchini, kuongeza imani ya wakulima katika mifumo ya usimamizi na kuimarisha mchango wa zao hilo katika kipato cha kaya na uchumi wa taifa.

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post