Kamanda wa polisi mkoni Shinyanga SACP. Janeth Magomi
akizungumza wakati wa kukabidhi mchango wa mifuko 16 ya saruji kwa niaba ya Jeshi la polisi wilayani Kishapu iliyotolewa kwa jeshi la Sungusungu Kata ya Maganzao kwa ajili ya kuunga mkono ujenzi wa jengo la ofisi Oktoba 28,2026
Kamanda wa polisi wilayani Kishapu mkoani Shinyanga SP. Ester Gesogwe akizungumza wakati wa kukabidhi mchango wa mifuko 16 ya saruji iliyotolewa na Jeshi la polisi wilayani humo kwa jeshi la Sungusungu Kata ya Maganzao kwa ajili ya kuunga mkono ujenzi wa jengo la ofisi Oktoba 28,2026
Na Sumai Salum- Kishapu
Jeshi la Polisi wilayani Kishapu, mkoani Shinyanga, limeunga mkono ujenzi wa Ofisi ya Sungusungu Kata ya Maganzo kwa kuchangia mifuko 16 ya saruji huku likiahidi kushirikiana katika ujenzi huo zaidi na Sungusungu kusimamia ujenzi huo hadi utakapokamilika.
Akizungumza wakati wa kukabidhi mchango huo Oktoba 28,2026 kwa niaba ya Jeshi la Polisi wilayani humo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP. Janeth Magomi, amewapongeza wananchi wa Maganzo kwa juhudi zao za kuimarisha ulinzi na usalama huku akiahdisi kutoa matofali 1,000 na akiwataka kuendelea kudumisha amani na utulivu, hususan katika kipindi cha mwisho wa mwaka.
Magomi amewataka wananchi kutokubali kushawishiwa na makundi yanayoweza kuvuruga amani, huku akisisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kuwalea watoto na vijana katika misingi mizuri ya maadili, imani, mila na desturi zisizokandamiza haki za wengine.
Aidha, ameendeleza kampeni ya *Ongea na Kamanda*, akiwahimiza wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na viashiria vyake kwa Jeshi la Polisi, pamoja na kutunza miundombinu ya Serikali na kushirikiana katika kulinda usalama wa raia na mali zao.
Katika hatua nyingine, Kamanda Magomi alikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Sungusungu katika kata hiyo na kuahidi kuchangia matofali 1,000 ili kusaidia kukamilika kwa mradi huo hukuakikubali ombi la viongozi wa Sungusungu la kuwa msimamizi wa jengo hilo, hatua inayolenga kuunga mkono juhudi za jamii katika kuimarisha shughuli za ulinzi shirikishi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kishapu, SP Ester Gesogwe, amesema Sungusungu ni kundi muhimu linaloshirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi katika kuzuia na kudhibiti uhalifu, hivyo mchango huo ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya usalama.
Naye Diwani wa Kata ya Maganzo, Mhe. Hamza Tandiko, amechangia Shilingi 500,000 taslimu kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hiyo na kuahidi kuendelea kuchangia kadiri ujenzi utakavyoendelea. Pia, amewawezesha Sungusungu wa Kijiji cha Ikonongo kupata fedha za kuanzia kwa ajili ya kufungua akaunti.
“Ninawasihi wananchi kuendelea kuchapa kazi kwa bidii ili kuinua uchumi wa Kata ya Maganzo na kukuza uchumi wa kaya na uchumi jumuishi unaowanufaisha wananchi wote,” amesema Tandiko.
Akiwasilisha taarifa ya ujenzi huo, Kamanda Mkuu Mwanamke wa Sungusungu Kata ya Maganzo, Tayaya Rashidi, amesema eneo la ujenzi limetolewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kata hiyo hivyo jengo hilo litakuwa na vyumba viwili vya ofisi, ukumbi wa mikutano na matundu nane ya vyoo, likiwa na makadirio ya gharama ya Shilingi milioni 33.5.
Amesema lengo la ujenzi huo ni kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao kupitia ushirikiano wa Sungusungu na Jeshi la Polisi, pamoja na kuweka mazingira rafiki kwa wananchi kuwasilisha shida, malalamiko na taarifa zao katika ofisi maalumu.
Viongozi wa Sungusungu wameishukuru Jeshi la Polisi wilayani Kishapu kwa msaada huo, huku wakitoa pongezi kwa askari wa Polisi Kata ya Maganzo, Afande Salvatory, na Mkuu wa Polisi Maganzo, Afande Maftah, kwa ushirikiano wao katika kuimarisha ulinzi na usalama katika eneo hilo.
Kupitia hafla hiyo Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa soko la Maganzo ameahidi kuwa yeye na wafanyabiashara hao watachangia mifuko mitano ya saruji na Sadick Mohamed afisa usafirishaji wa taka za sokoni akiahidi kutoa Tsh. 100, 000.
Mkuu wa Polisi Kata ya Maganzo Afande Issa Maftah
Polisi Kata ya Maganzo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Ins. Salvatory Sakondo akisoma taarifa ya Kata hiyo
Matendaji wa Kata ya Maganzo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Stephen Yalomba
Mtemi wa sungusungu Kata Maganzo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Kulwa Paul
Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Kishapu, SP Chacha M. Mwita
Kijana Alexander Amos mkazi wa Magazno aliyeamua kubadilika kutoka kwenye tabia mbaya za uhalifu na sasa akiahidi kuwa balozi wa amani
Msingi wa jengo hilo lenye vyumba viwili vya ofisi, ukumbi wa mikutano na matundu nane ya vyoo, likiwa na makadirio ya gharama ya Shilingi milioni 33.5
Post a Comment