TANZANIA NA SDIG ZAJADILI UTEKELEZAJI WA MRADI WA LIGANGA NA MCHUCHUMA NA FURSA ZAIDI ZA UWEKEZAJI NCHINI

-Waziri Kapinga akutana na wawekezaji wa Kampuni ya ShuDao Investment Group Co. Limited (SDIG) wanaotekeleza mradi wa Mchuchuma na Liganga nchini China.

-Serikali ya Tanzania na SDIG zakubaliana kukamilisha ujenzi wa miradi hiyo ifikapo Julai 2030.

-SDIG yaonesha nia ya kupanua uwekezaji nchini kwa kujenga viwanda vya kuunganisha mabasi na kuzalisha mbolea.

- Mradi wa Mchuchuma na Liganga ni miongoni mwa miradi saba ya kielelezo inayotarajiwa kuchangia kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.

CHENGDU CHINA,

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Salvio Kapinga (Mb.), akiambatana na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Deodatus P. Mwanyika (Mb.), amefanya kikao na uongozi wa juu wa Kampuni ya ShuDao Investment Group Co. Limited (SDIG) katika makao makuu ya kampuni hiyo jijini Chengdu, China, kwa lengo la kuharakisha utekelezaji wa Mradi Unganishi wa Makaa ya Mawe wa Mchuchuma na Chuma cha Liganga.

Katika kikao hicho kilichofanyika Novemba 17, 2026, Serikali na SDIG zimekubaliana kuhakikisha ujenzi wa Mradi wa Mchuchuma na Liganga unakamilika ifikapo Julai 2030, huku zikiendelea na hatua za maandalizi ikiwemo kukamilisha mapitio ya taarifa ya upembuzi yakinifu, Moduli ya Fedha ya Pamoja, mikataba ya mradi, tathmini ya athari za kimazingira na kijamii (EIA) pamoja na usanifu wa mradi. Pande hizo zinatarajia kusaini makubaliano katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2026/2027.

Mhe. Kapinga amesema Mradi wa Mchuchuma na Liganga ni miongoni mwa miradi saba ya kielelezo ambayo Tanzania inaitegemea katika kufikia uchumi wa dola trilioni moja kupitia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050, Uwekezaji wa SDIG katika mradi huo unatokana na mazungumzo yaliyofanyika kati ya Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa China, Xi Jinping, wakati wa ziara ya kiserikali ya Rais Samia nchini China Novemba 2022.

Mbali na Mradi wa Mchuchuma na Liganga, SDIG imeonesha dhamira ya kuongeza uwekezaji wake nchini kwa kuzungumzia juu ya fursa zingine zilizopo katika sekta ya kilimo, sekta ya uchukuzi, uwekezaji katika sekta za nishati na madini pamoja na uwekezaji unaohusu maeneo ya viwanda na logistiki. Nia ya Uwekezaji huo ni kuongeza ajira, mapato na kupanua fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali.

Mhe. Kapinga yupo nchini China katika ziara ya kikazi iliyoanza Novemba 15 na inayotarajiwa kuhitimishwa Novemba 21, 2026, ziara hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na China, pamoja na kuvutia uwekezaji zaidi hatua hiyo inatarajiwa kuchochea maendeleo ya viwanda, kuongeza ajira na kukuza uchumi wa Taifa.

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post