
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeeleza dhamira yake ya kuendelea kusimamia mfumo wa kodi unaovutia uwekezaji, kukuza biashara na kuwezesha ukuaji wa uchumi wa Taifa, kwa kuzingatia misingi ya haki, usawa na uwazi katika usimamizi wa kodi.
Hayo yameelezwa na Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, katika mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Mhe. Noel Emmanuel Kaganda, yaliyolenga kuimarisha ushirikiano katika masuala ya kodi, biashara na uwekezaji.
Akizungumza katika mazungumzo hayo, Balozi Kaganda ameipongeza TRA kwa mafanikio yaliyopatikana katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali, akitambua juhudi zinazofanywa na Mamlaka katika kuboresha mifumo ya kodi na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Korea Kusini.
Akizungumza kuhusu juhudi za TRA, Kamishna Mkuu Mwenda ameeleza kuwa Mamlaka inaendelea kuboresha mifumo na huduma zake kwa kutumia teknolojia, kurahisisha taratibu za kikodi na kutoa elimu kwa walipakodi ili kuhakikisha mazingira ya kodi yanawezesha biashara na uwekezaji, sambamba na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Aidha, Bw. Mwenda amesisitiza utayari wa TRA kuendeleza ushirikiano na Korea Kusini katika maeneo yenye maslahi ya pamoja, ikiwemo kubadilishana uzoefu na kujifunza mifumo bora ya usimamizi wa kodi, hatua itakayochangia kuimarisha mazingira ya uwekezaji, kukuza biashara na kuongeza mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.









إرسال تعليق