MAAJABU YA MLIMA KIDENGE YATAJWA KIVUTIO KIKUU TAMASHA LA SAME UTALII FESTIVAL

Na Mwandishi wetu


Katika ukanda wa milima ya Pare Kusini, ndani ya Kata ya Vunta wilayani Same, Mkoa wa Kilimanjaro, kuna kivutio cha kipekee cha asili kinachozidi kuvutia macho na hisia za wengi—Mlima Kidenge. Ingawa si mkubwa kwa kimo, mlima huu umejipatia umaarufu kutokana na maajabu yake ya kiasili, historia ya kimila, na simulizi zinazorithishwa kizazi hadi kizazi miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.


Kivutio kikubwa kinachobeba hadhi ya mlima huu ni pango maarufu lijulikanalo kwa jina la Kangulu kwa lugha ya Kipare. Ndani na nje ya pango hilo kuna mtandao wa kona nyingi na njia zinazofanya eneo hilo la mwinuko mzuri kufanana na ukuta wa china ya maajabu unaopatikana katika nchi ya China (Great Wall of China). Muundo huo wa kipekee umeibua hamasa kwa watafiti na watalii wanaopenda kuchunguza maumbile yasiyo ya kawaida.


Lakini zaidi ya muonekano wake, Mlima Kidenge una siri nyingine ya kushangaza—uwepo wa wanyama wa kufugwa kama ng’ombe, mbuzi, kondoo na punda wanaoishi ndani ya pango hilo. Kinachowashangaza wengi ni kwamba wanyama hao hawajulikani walikotoka, lakini huonekana wakitoka nje kujitafutia chakula na baadaye kurudi pangoni humo kana kwamba wana makazi ya kudumu.
Aidha, eneo hili lina utajiri wa madini mbalimbali, hususan madini yanayojulikana kama lupia, ambayo yanapatikana kwa wingi. Licha ya uwepo wake, jamii ya wenyeji imekuwa na utamaduni wa kulinda rasilimali hizo kwa misingi ya imani za jadi, ambapo kuchukua madini hayo bila ruhusa huchukuliwa kuwa ni mwiko mkubwa.

Kwa mujibu wa simulizi za wazee wa eneo hilo, Mlima Kidenge ulikuwa ukitumika kwa shughuli za kimila zikiwemo tambiko maalum zilizolenga kuomba mvua, ulinzi wa jamii na ustawi wa mifugo. Hivyo basi, mlima huu si tu kivutio cha kijiografia bali pia ni hazina ya utamaduni na historia ya Wapare.

Mbali na historia yake ya kimila, mlima huu pia una mchango mkubwa katika uhifadhi wa mazingira. Uoto wa asili unaozunguka Mlima Kidenge husaidia kuhifadhi vyanzo vya maji na kuwa makazi ya viumbe hai mbalimbali, hali inayoufanya kuwa muhimu si tu kwa utalii bali pia kwa maisha ya jamii inayouzunguka.

Wakazi wa Kata ya Vunta wameanza kuona fursa mpya kupitia mlima huu, hususan katika sekta ya utalii wa ndani. Vijana na vikundi vya kijamii wanahamasishwa kushiriki katika shughuli za uongozi wa watalii, uhifadhi wa mazingira na uendelezaji wa utamaduni wao ili kunufaika kiuchumi na rasilimali hiyo ya kipekee.

Kutokana na upekee huo, Mlima Kidenge umeingizwa katika orodha ya vivutio vya utalii vinavyotambuliwa kitaifa, na unatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya maonesho katika Tamasha la Same Utalii Festival Season 3 litakalofanyika kuanzia tarehe 10 hadi 12 katika Wilaya ya Same.

Tamasha hilo linatarajiwa kuvutia wageni kutoka maeneo mbalimbali na kutoa fursa ya kuitangaza zaidi hazina hii adhimu ya asili.

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post