
Na Mwandishi Wetu
Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) imeonyesha wazi kumuunga mkono aliyekuwa mbunge wa Kawe, Halima Mdee, baada ya kutangaza kuwa ipo tayari kumpokea tena ndani ya chama hicho na kumpa nafasi ya kushiriki shughuli mbalimbali za kisiasa na kichama zinazoendelea nchini.
Katika kikao chake, Kamati Kuu imeeleza kuwa kulikuwa na mazingira yaliyoifanya CHADEMA kutomtendea haki Halima Mdee licha ya mchango wake mkubwa katika mapambano ya haki, demokrasia na utetezi wa wananchi ndani na nje ya Bunge.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, viongozi wa juu wa chama wamekubaliana kuwa Mdee amebaki kuwa mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa na mpambanaji wa kweli asiyeogopa kusimamia maslahi ya wananchi, jambo lililosababisha Kamati Kuu kumuangukia na kuona umuhimu wa kumkaribisha tena ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Hata hivyo, hali imekuwa tofauti kabisa kwa aliyekuwa mchungaji na mwanasiasa wa CHADEMA, Mchungaji Peter Msigwa, ambapo Kamati Kuu imeweka msimamo mkali dhidi yake na kueleza kuwa haipo tayari hata kujadili suala la kurejea kwake ndani ya chama.
Akizungumza na waandishi wa habari leo kwa njia ya mtandao, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, alisema chama hakijapokea wala kuridhia barua yoyote ya Msigwa ya kuomba kurejea CHADEMA, huku akisisitiza kuwa hatua alizochukua mwanasiasa huyo zimeonekana kuwa ni usaliti mkubwa kwa chama na wanachama wake.
“Kurudi kwa Msigwa ndani ya CHADEMA ni zaidi ya usaliti,” alisema Mnyika kwa msisitizo huku akieleza kuwa chama hakiwezi kufumbia macho vitendo vinavyokwenda kinyume na misingi, maadili na harakati za kidemokrasia ambazo wanachama wamekuwa wakizipigania kwa muda mrefu.
Kauli hiyo imezua mjadala mkubwa ndani na nje ya CHADEMA, huku baadhi ya wanachama wakitafsiri hatua ya kumkaribisha Halima Mdee kama ishara ya maridhiano mapya, lakini wengine wakiona msimamo dhidi ya Msigwa kuwa ujumbe mzito kwa viongozi wanaotuhumiwa kwenda kinyume na misingi ya chama.
Wachambuzi wa siasa wanasema hatua hiyo inaweza kuwa sehemu ya mkakati wa CHADEMA kujijenga upya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao kwa kuwarejesha baadhi ya wanasiasa wenye ushawishi huku ikiwabana wale wanaoonekana kukisaliti chama hicho.
Mpaka sasa, Halima Mdee hajatoa kauli rasmi kuhusu uamuzi huo wa Kamati Kuu, huku upande wa Mchungaji Msigwa nao ukiendelea kuwa kimya kufuatia tamko kali lililotolewa na uongozi wa chama hicho.
Post a Comment