MAADHIMISHO YA SIKU YA FAMILIA 2026 KUONGEZWA NGUVU NA WADAU WA MTOTO


Na Dotto Kwilasa,Dodoma



Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imetangaza kuwa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia kwa mwaka 2026 yatafanyika rasmi tarehe 30 Juni 2026 kwa kuunganishwa na maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, hatua inayolenga kuimarisha juhudi za pamoja katika masuala ya familia, malezi na makuzi ya watoto nchini.


Akzungumza Mei 14, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima amesema kuwa Tanzania imeendelea kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Familia kila mwaka kupitia shughuli mbalimbali zinazolenga kuhamasisha umuhimu wa familia katika maendeleo ya jamii na taifa.


Kwa mujibu wa Waziri huyo, maadhimisho ya mwaka huu yataongozwa na kaulimbiu isemayo “Mtoto ni Malezi; Msingi wa Familia Bora kwa Taifa Imara”, ambayo inalenga kusisitiza umuhimu wa malezi bora ya watoto kuanzia kipindi cha ujauzito hadi wanapofikisha umri wa miaka 18.


Ameeleza kuwa kaulimbiu hiyo pia inalenga kuikumbusha jamii wajibu wake katika kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira yenye maadili mema, upendo, ulinzi na usalama ili kujenga kizazi chenye msingi imara wa maendeleo.


“Maendeleo endelevu ya kiuchumi, kijamii na kisiasa ya taifa letu yatategemea namna watoto wanavyolelewa na kukuzwa kwa kuzingatia maadili pamoja na mila na desturi njema za Kitanzania,” alisema Dkt. Gwajima.


Aidha, Wizara hiyo imewataka wananchi kuanza kutafakari nafasi ya familia katika malezi na makuzi ya watoto kuanzia Mei 15, 2026 huku ikiendelea kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari kuelekea kilele cha maadhimisho hayo kitakachofanyika Juni 30, 2026.


Waziri Gwajima alisisitiza kuwa uwekezaji katika malezi ya watoto ni msingi muhimu wa kujenga familia bora na taifa imara kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.


Maadhimisho hayo yanatarajiwa kushirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo, taasisi za serikali na zisizo za serikali pamoja na jamii kwa ujumla katika kuendeleza kampeni ya kuhamasisha malezi chanya nchini Tanzania.

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post