Na Mwandishi wetuJeshi la Polisi Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga kupitia Dawati la Jinsia limeendelea kuimarisha mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa kutoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Somagedi iliyopo kijiji cha Wimate, kata ya Somagedi wilayani humo.
Elimu hiyo imelenga kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia, namna ya kujilinda pamoja na umuhimu wa kuzingatia maadili, nidhamu na elimu kwa ajili ya kujenga jamii salama na yenye ustawi.
Akitoa elimu hiyo, Sajini Clemence Mgaya kutoka Dawati la Jinsia Jeshi la Polisi Kishapu amesema vijana na wanafunzi wanapaswa kuwa mstari wa mbele kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyosababisha madhara makubwa kwa watoto, wanawake na jamii kwa ujumla.
Katika mada zilizowasilishwa, wanafunzi walifundishwa kuhusu maana ya ukatili, aina mbalimbali za ukatili, mbinu za kujikinga dhidi ya ukatili pamoja na madhara yatokanayo na vitendo hivyo katika maisha yao ya kila siku.
Aidha, Sajini Mgaya ametoa elimu kuhusu madhara ya utoro shuleni, akieleza kuwa wanafunzi wanaokosa masomo mara kwa mara hujikuta katika mazingira hatarishi yanayoweza kusababisha kujiingiza kwenye vitendo vya ukatili, matumizi ya dawa za kulevya, mimba za utotoni na kushindwa kufikia ndoto zao za maisha.
Mgaya amesisitiza wanafunzi kutoa taarifa mapema wanapokutana na vitendo vya ukatili na kushirikiana na walimu, wazazi pamoja na vyombo vya dola ili kuhakikisha mazingira ya shule na jamii yanakuwa salama kwa kila mtoto.
Kwa upande wao, baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Somagedi wamesema elimu hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwao kwani imewawezesha kutambua haki zao na namna ya kujikinga dhidi ya vitendo vya ukatili.
“Mafunzo haya yametufungua macho. Tumeelewa kuwa ukatili si jambo la kuficha na sasa tunajua namna ya kutoa taarifa tunapoona au kufanyiwa vitendo vya ukatili,” amesema mmoja wa wanafunzi aliyeshiriki mafunzo hayo.
Mwanafunzi mwingine amesema elimu hiyo itawasaidia kuzingatia masomo na kujiepusha na utoro ambao unaweza kuwapelekea kuingia kwenye makundi mabaya au vitendo vinavyoweza kuharibu maisha yao ya baadaye.
Naye mmoja wa walimu wa shule hiyo amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuendelea kutoa elimu kwa wanafunzi akisema hatua hiyo inasaidia kujenga mazingira salama ya kujifunzia na kuwafanya wanafunzi kuwa na uelewa mpana kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia.
“Elimu hii ni muhimu sana kwa watoto wetu kwani inawasaidia kujitambua, kujiamini na kujua namna ya kujilinda. Tunaamini itasaidia kupunguza vitendo vya ukatili na kuongeza nidhamu shuleni,” amesema mwalimu huyo.









Post a Comment