RAS SHINYANGA APONGEZA CHAMA CHA SKAUTI KWA MALEZI MAZURI YA VIJANA

Na Ofisi ya Skauti - Shinyanga


Katibu Tawala wa mkoani Shinyanga,CP. Salum Hamdun amefanya kikao maalum na viongozi wa Skauti Mkoani humo na wageni walimu wa Skauti kutoka Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha. Wageni hao waliambatana na mwenyeji wao, Kamishna wa Skauti Mkoa wa Shinyanga, ALT Mussa M. Chama.


Akizungumza wakati wa kikao hicho Mei, 22,2026 ofsini kwake, Cp Hamdun amewakaribisha rasmi wageni hao kutoka Ngorongoro na kutoa maelekezo, ushauri pamoja na nasaha mbalimbali kuhusu umuhimu wa Skauti katika jamii na maendeleo ya taifa kwa ujumla.


Aidha, amepongeza uongozi wa Skauti Mkoa wa Shinyanga unaoongozwa na ALT Mussa M. Chama kwa namna wanavyoendesha shughuli zao kwa ufanisi mkubwa na kuendelea kuwa mfano bora wa malezi kwa vijana.


"Kipekee nikupongeze Kamishna Chama, kwa uongozi wako thabiti unaozingatia ushirikiano na ushirikishwaji, hali iliyowezesha mapokezi mazuri kwa wageni kutoka Mkoa wa Arusha".


Cp. Hamdun alisisitiza kuwa Skauti ina mchango mkubwa katika kujenga taifa lenye vijana wenye nidhamu, uzalendo na maadili mema. Alieleza kuwa katika kipindi hiki cha mabadiliko makubwa ya teknolojia na mitindo ya maisha, taasisi ya Skauti inaendelea kuwa mwongozo muhimu kwa vijana katika kufuata njia sahihi zenye manufaa kwa jamii.


Vilevile, alikumbusha kuwa mlezi wa Skauti nchini ni Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku Mkoa wa Shinyanga ukiwa chini ya ulezi wa Mkuu wa Mkoa, Mhe. Mboni Mhita. Amesema hali hiyo inaonesha wazi nafasi na umuhimu wa Skauti kama taasisi yenye misingi imara ya nidhamu, uzalendo na ujenzi wa taifa.


Kwa upande wa fursa, Cp. Hamdun alibainisha kuwa wanachama wa Skauti wataendelea kupewa kipaumbele katika nafasi mbalimbali za ajira na teuzi kutokana na mafunzo ya nidhamu, uzalendo na moyo wa kujitolea waliyonayo. Amesisitiza kuwa mafanikio hayo yataongezeka zaidi endapo vijana wa Skauti wataendelea kulitumikia Taifa kwa moyo wa dhati na uwajibikaji.

Afisa elimu Mkoani watu wazima akimwakilisha Afisa Elimu mkoani humo, Mwl. Dedan Lutazikwa alisema Skauti ni chombo muhimu katika malezi ya vijana wenye nidhamu, uzalendo, kujitolea na uwezo wa kujitegemea. 


"Kupitia skauti, wanafunzi hujifunza maadili mema, uongozi, ushirikiano pamoja na stadi za maisha ambazo huwasaidia kuwa raia bora wa sasa na baadaye. Mkoa tunaendelea kuhamasisha shule na jamii kuunga mkono shughuli za skauti kwa kuwa zinachangia kukuza elimu ya vitendo na kujenga taifa lenye vijana wenye maadili na uwajibikaji.” aliongeza Lutazikwa



Kwa upande wake, Kamishna wa Skauti Wilaya ya Ngorongoro Haji Mzee, alimshukuru CP. Salum Hamdun pamoja na uongozi wa Mkoa wa Shinyanga kwa mapokezi mazuri na ushirikiano waliouonesha kwa wageni hao. Alisema ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwa walimu wa Skauti kutoka Ngorongoro kutokana na fursa ya kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu mbalimbali za uongozi na kuimarisha mahusiano kati ya Skauti wa mikoa hiyo miwili.


Kwa upande wake, Kamishna wa Skauti Mkoa wa Shinyanga, ALT. Mussa M. Chama, alimshukuru CP. Salum Hamdun kwa kuwapokea na kuwapa nafasi ya kufanya kikao hicho muhimu kilicholenga kuimarisha mahusiano na ushirikiano ndani ya taasisi ya Skauti huku akipongeza ziara hiyo ya siku mbili mkoani Shinyanga.


"Ujio wa walimu wa Skauti kutoka Wilaya ya Ngorongoro ni ishara ya mshikamano na dhamira ya pamoja ya kuendeleza malezi bora kwa vijana nchini. Aidha sisi Skauti Mkoa wa Shinyanga tutaendelea kushirikiana na mikoa mingine katika kubadilishana uzoefu, mafunzo na mbinu mbalimbali zitakazosaidia kukuza nidhamu, uzalendo na uongozi bora kwa vijana wa Kitanzania" ameongeza Alt. Chama.


Kikao hicho kimeendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya viongozi wa Serikali na taasisi ya Skauti katika kuendeleza malezi bora ya vijana nchini pamoja na kukuza maadili mema kwa kizazi cha sasa na kijacho.







0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post