AJALI YA BASI KAHAMA WATU SITA WAFARIKI, WATANO WAJERUHIWA


Safari ya abiria waliokuwa wakielekea mkoani Geita imekatishwa ghafla baada ya basi la kampuni ya OG Classic, lenye namba T985 DXL aina ya TATA, kupata ajali katika eneo la Wendele, Manispaa ya Kahama, na kusababisha vifo vya watu sita huku wengine watano wakijeruhiwa.


Ajali hiyo imetokea leo Jumamosi, Juni 20, 2026, majira ya saa 12:00 asubuhi, wakati basi hilo lilipokuwa likisafiri kutoka Kahama kuelekea Geita.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa dereva wa basi alifanya jaribio la kulipita lori lililokuwa likielekea Masumbwe bila kuhakikisha mazingira yalikuwa salama.


Amefafanua kuwa baada ya kuanza kulipita lori hilo, dereva alishindwa kulimudu basi kutokana na mwendo kasi, likagonga ukingo wa barabara, kisha likarudi barabarani na kugonga tela la lori kabla ya kupinduka.


"Taarifa za awali zinaonyesha dereva alikuwa katika mwendokasi. Alipojaribu kulipita lori bila tahadhari, aligonga ukingo wa barabara, akapoteza mwelekeo na hatimaye kugonga tela la lori kabla ya basi kupinduka," amesema Kamanda Magomi.


Majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu, huku miili ya waliofariki ikihifadhiwa kusubiri utambuzi wa ndugu na taratibu za mazishi.


Jeshi la Polisi limetoa wito kwa madereva wote kuzingatia sheria za usalama barabarani, hususan kuepuka mwendokasi na kufanya maamuzi ya tahadhari wanapolipita magari mengine, ili kupunguza ajali zinazogharimu maisha ya watu.

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post