CG MWENDA AWATAKA WASTAAFU WA TRA KUWA MABALOZI WA KODI

  

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda amewataka watumishi wastaafu wa Mamlaka hiyo kuwa Mabalozi wa Kodi ili kuongeza uelewa wa umuhimu wa kulipa kodi kwa jamii na kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari. 

Ameyasema hayo Juni 26, 2026 jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuwashukuru Wastaafu kwa mchango wao wa kuijenga TRA ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka hiyo tangu kuanzishwa kwake na utolewaji wa Tuzo za Rais kwa Mlipakodi Bora zinazotarajiwa kutolewa Julai Mosi mwaka huu kwenye ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam. 

Akizungumza katika hafla hiyo Kamishina Mkuu amesema TRA inatambua na kuthamini mchango wa wastaafu hao kwa kujenga msingi imara wa mafanikio ya miaka 30 ya taasisi hiyo.

Amesema mafanikio yaliyofikiwa leo hayawezi kutenganishwa na kazi kubwa iliyofanywa na watumishi waliowahi kuitumikia taasisi hiyo.

“Leo tumewaalika ili kuwashukuru kwa kazi kubwa mliyoifanya katika kipindi cha miaka 30 ya TRA, Tusingekuwa hapa kuadhimisha mafanikio haya bila mchango wenu mkubwa mlipokuwa mnalitumikia taifa,” amesema Mwenda.

Amesema Serikali imepiga hatua kubwa kiuchumi na katika ukusanyaji wa mapato, na kwamba mafanikio hayo yameiwezesha nchi kuongeza uwezo wa kujitegemea kwa kiasi kikubwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Wastaafu hao Bw. Julius Ceazar amemshukuru Kamishna Mkuu Mwenda kwa kukutana nao na kuipongeza TRA kwa kuendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji wa kodi unaoijengea rekodi mpya kila siku.

Amesema wanajivunia kuwa miongoni mwa watumishi waliowahi kufanya kazi TRA na kuiwezesha kufikia miaka 30 ya mafanikio ambayo yanaiwezeshq Mamlaka hiyo kuwa na mchango mkubwa katika mapato ya  Serika.

"Kwa umoja wetu tunajivunia kuwa sehemu ya miaka 30 ya TRA na sasa tumeshuhudia ukaribu mkubwa uliopo baina ya TRA na Walipakodi hali ambayo imewafanya Walipakodi walipe kodi kwa hiari" amesema Ceazar.

Wastaafu hao wameshukuru kwa kupatiwa Ubalozi wa Kodi na kuahidi kutekeleza jukumu hilo kwa uaminifu na uadilifu.






0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post