
Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema hakuna Mtanzania anayepaswa kuambiwa kuwa anadaiwa sehemu ya deni la Taifa, akisisitiza kuwa mikopo inayochukuliwa ni deni la Serikali kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo na si deni la mtu mmoja mmoja.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Juni 28, 2026, Msigwa amesema kumekuwa na upotoshaji unaolenga kuwafanya wananchi waamini kila Mtanzania anabeba deni binafsi kutokana na mikopo ya Serikali, jambo alilosema si sahihi kwa mujibu wa namna fedha za umma zinavyosimamiwa.
"Ni muhimu Watanzania wakaelewa jambo hili,deni hili ni la Serikali, si la mtu mmoja mmoja,hakuna Mtanzania anayekopeshwa halafu baadaye akaambiwa alipe sehemu yake binafsi ya deni la Taifa," amesema.
Amefafanua kuwa Serikali hukopa fedha kama chombo cha kufadhili bajeti na miradi ya maendeleo inayowanufaisha wananchi wote, ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Julius Nyerere, barabara, viwanja vya ndege, miradi ya maji, hospitali, shule na miundombinu mingine.
Msigwa amesema mikopo hiyo haiendi kwenye matumizi binafsi wala kugawanywa kwa watu, bali huwekezwa kwenye miradi inayoongeza uwezo wa uchumi wa nchi na kuboresha huduma za kijamii.
Amesema hadi kufikia Machi 2026, deni la Serikali lilikuwa Shilingi trilioni 114.34, lakini tathmini ya uhimilivu wa deni imeonyesha kuwa Tanzania bado ipo ndani ya viwango vinavyokubalika kimataifa, jambo linaloonyesha nchi ina uwezo wa kuhudumia madeni yake bila kuhatarisha uchumi.
"Tunakopa kwa sababu tunakopesheka. Hakuna taasisi ya fedha duniani inayotoa mkopo kwa nchi isiyo na uwezo wa kulipa,Kama ilivyo kwa mtu anayekwenda benki, lazima akidhi vigezo kabla ya kukopeshwa," amesema.
Msigwa amewataka wananchi kupuuza kauli zinazodai kila Mtanzania anadaiwa mamilioni ya shilingi kutokana na deni la Taifa, akisema kauli hizo zinapotosha uelewa wa wananchi kuhusu namna Serikali inavyosimamia fedha za umma.
Amesisitiza kuwa mjadala unaopaswa kufanywa si kuhesabu deni kwa kila mwananchi, bali kuangalia kama fedha zilizokopwa zimeleta matokeo yanayoonekana kupitia miradi ya maendeleo, ukuaji wa uchumi na uboreshaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Msigwa, Serikali itaendelea kutumia mikopo kwa uwajibikaji na kuelekeza fedha hizo kwenye miradi yenye tija ili kuharakisha maendeleo ya Taifa na kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.




Post a Comment