OWM NA SKAUTI DODOMA MGUU SAWA USIMAMIZI WA MAAFA

 

Na Mwandishi Wetu, Dodoma.

Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na wenye Ulemavu imefanya mafunzo ya usimamizi wa maafa kwa Uongozi wa Skauti Mkoa wa Dodoma leo Juni  29, 2026 jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (SBUU) Brig. Jen Hosea Ndagala, ameipongeza Skauti Tanzania kwa ushirikiano ambao wanaoutoa wakati wote katika kushughulikia matukio mbalimbali ambayo yamekua yakitokea nchini, hivyo mafunzo hayo ni sehemu ya kujiweka sawa juu ya kuimarisha namna bora ya mashirikiano haya.

Brig. Jen Ndagala ameongeza kuwa, Mfumo wa usimamizi wa maafa nchini ni mfumo unaoanzia ngazi ya Taifa hadi Kijiji, hivyo Mfumo huo ukifuatwa utasaidia kupunguza athari za majanga.

"Kama kamati zote katika Mfumo huu zitafanya kazi kama inavyotakiwa hatutegemei kuwa na maafa makubwa, kwani majanga mengine huwezi kuyazuia lakini kuna mambo kadhaa ya kuyazuia, na kuna mengine yakitoea unapunguza maafa kwa binadamu, miundombinu na maswala mengine hususani shughuli za kijamii na uchumi na kulinda maendeleo ambayo nchi imeshayapata ", ameeleza Brig. Jen Ndagala.

Aidha, Brig. Jen Ndagala amewataka washiriki wa mafunzo hayo kutoka skauti Mkoa wa Dodoma kutumia mafunzo hayo na  kuwa Mabalozi ili kuelimisha na  kutahadharisha jamii hatua mahususi za kuchukua tahadhari za mapema, kujikinga au kupunguza madhara ambayo yanaweza kujitokeza ili kuendelea kuhakikisha taifa linakuwa salama na matukio ya Maafa.

Nae, Kamishna wa Skauti Mkoa wa Dodoma Bi. Salama Katunda ametumia Mafunzo hayo kudhihirisha adhma ya skauti ya kuendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura katika kujiandaa, kutoa elimu na kukabiliana na maafa nchini .

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mkurugenzi msaidizi Idara ya Menejimenti ya Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (SBUU) Bi. Jane Kikunya amesema kuwa, mafunzo hayo ni sehemu ya kuimarisha mashirikiano yaliyopo kati ya serikali na wadau mbalimbali katika usimamizi na uratibu wa maafa nchini na kusema Ofisi ya Waziri Mkuu iko tayari kuendeleza mashirikiano hayo.

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post