Na Mbuke Shilagi- KageraKamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera RPC, Barasius Chatanda, amewataka wazazi na walezi kuwa karibu zaidi na watoto wao ili kufahamu changamoto wanazopitia na kusaidia kutatua matatizo yanayoweza kusababisha maamuzi hatari.
Wito huo ameutoa leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya operesheni mbalimbali za kuimarisha ulinzi na usalama zilizofanyika mkoani humo kuanzia Mei 1 hadi Juni 16, 2026, ambapo watuhumiwa wa makosa mbalimbali walikamatwa.
RPC Chatanda amesema kauli hiyo kutokana na tukio la kusikitisha la mwanafunzi wa Kidato cha Tatu wa Shule ya Sekondari Bishop Kibila, iliyopo Kata ya Nyakato, Tarafa ya Bugando, Wilaya ya Bukoba, aliyefahamika kwa jina la Jovan Reveliani Jastinian, ambaye alikutwa amefariki dunia baada ya kujinyonga katika bweni alilokuwa akiishi.
Awali mwanafunzi huyo amebakizwa shuleni pamoja na wanafunzi wengine kwa ajili ya masomo ya ziada kutokana na kufanya vibaya katika mitihani, hali ambayo inadaiwa hakuiridhia na baadaye kuchukua uamuzi huo wa kusikitisha.
Aidha, RPC Chatanda amewahimiza watoto na wanafunzi kutoa taarifa kwa walimu, wazazi au wenzao wanapokumbana na changamoto zinazowasumbua ili kupata msaada mapema, Vilevile, amesisitiza umuhimu wa mawasiliano ya karibu kati ya wazazi na watoto wao ili kubaini mapema matatizo wanayokabiliana nayo wakiwa shuleni au katika mazingira ya jamii na hivyo kuzuia matukio yanayoweza kuhatarisha maisha yao.


Post a Comment