
Na mwandishi wetu, Dodoma
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) linatarajia kuandika historia mpya Juni 19, 2026 kwa kuhitimisha maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, huku likitarajia kuzindua kitabu maalumu kitakachobeba historia, mafanikio na mchango wake katika maendeleo ya viwanda, biashara na ustawi wa Watanzania.
Akizungumza jijini Dodoma kuhusu maandalizi ya kilele cha maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi, amesema hafla hiyo itafanyika katika ofisi za shirika hilo na inatarajiwa kuhudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka sekta za umma na binafsi.
Dkt. Katunzi amesema mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Salvio Kapinga (Mb), ambaye ataungana na viongozi, wadau na wananchi kusherehekea mafanikio ya nusu karne ya taasisi hiyo muhimu nchini.
Amesema sambamba na sherehe hizo, TBS itazindua kitabu maalumu cha miaka 50 kitakachoelezea safari ya shirika hilo tangu kuanzishwa kwake, hatua mbalimbali za maendeleo iliyopitia pamoja na mchango wake katika kuhakikisha bidhaa na huduma zinazotolewa nchini zinazingatia viwango vinavyotakiwa.
“Kitabu hiki kitakuwa sehemu ya kumbukumbu muhimu ya taifa. Kitaelezea historia ya TBS, mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 50 na kitakuwa rejea kwa vizazi vya sasa na vijavyo ili kuelewa mchango wa shirika katika maendeleo ya nchi,” amesema Dkt. Katunzi.
Ameeleza kuwa kwa kipindi cha miaka 50, TBS imeendelea kuwa mhimili muhimu katika kulinda afya na usalama wa watumiaji wa bidhaa mbalimbali, huku ikichochea ukuaji wa viwanda kwa kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinakuwa bora na zenye ushindani katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Dkt. Katunzi, mafanikio yaliyofikiwa na TBS katika kipindi hicho si ya shirika pekee bali ni matokeo ya ushirikiano mkubwa kati ya taasisi hiyo, wadau wa maendeleo, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla.
“Miaka 50 ya TBS ni mafanikio ya wadau wetu na jamii kwa ujumla. Tunawakaribisha wananchi na wadau wote kushiriki katika kilele cha maadhimisho haya ili kwa pamoja tuadhimishe safari hii ya mafanikio,” amesema.
Maadhimisho hayo yanatarajiwa kuwa fursa ya kutafakari mchango wa TBS katika maendeleo ya taifa, huku yakitoa mwanga wa matarajio na mwelekeo wa shirika hilo katika kuendelea kuimarisha ubora wa bidhaa na huduma kwa manufaa ya Watanzania na uchumi wa nchi.
Post a Comment