Na Sumai Salum – Kishapu
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi ameongoza baadhi ya wakuu wa Tasasisi na mamia ya wananchi wa Wilaya hiyo, leo Jumamosi Julai 11, 2026, kushiriki mazoezi ya pamoja (jogging).Mazoezi hayo yamewakutanisha wanachama wa vikundi vya Jogging vya Kishapu na Ukenyenge, yakilenga kudumisha Amani na kuimarisha afya, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa wananchi.
Akizungumza baada ya mazoezi hayo, Mhe. Masindi amesema kufanya mazoezi ya pamoja ni njia muhimu ya kuendeleza amani, umoja na upendo katika Wilaya ya Kishapu, huku akiwahimiza wananchi kuendelea kushiriki shughuli zinazojenga afya na kuimarisha mahusiano ya kijamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Emmanuel Johnson, amesema mazoezi ni sehemu muhimu ya kujenga afya bora na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku. Amewahimiza wananchi kuyaweka mazoezi katika ratiba zao ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza na kuishi maisha yenye afya.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi
Sambamba na mazoezi hayo, Wilaya ya Kishapu imeanza Bonanza la Veteran Sabasaba 2026 lenye kaulimbiu isemayo, "Amani na Utulivu Kishapu ni Tunu ya Taifa." Bonanza hilo linafanyika kwa siku mbili, Julai 11–12, 2026 lililoratibiwa na Kishapu Verterani na kulindima katika Viwanja vya Shule ya Msingi Buduhe , likizikutanisha timu mbalimbali za veterani kutoka ndani na nje ya Mkoa.
"Timu zinazoshiriki Bonanza la Veteran Sabasaba 2026, Kishapu Veteran, Shinyanga Veteran, Shy Town Veteran, Simiyu Veteran, Biashara Veteran, Mwanza Veteran, Shy Talent Veteran na Musoma Veteran"Amesema Mwenyekiti wa Kishapu Verteran Sostenes Amas
Ratiba ya michezo inaonesha mechi mbalimbali zitakazochezwa kwa siku mbili, huku mashabiki wakitarajiwa kushuhudia ushindani mkubwa sambamba na kuendelea kuhamasisha amani, mshikamano na afya kupitia michezo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Emmanuel Johnson
Post a Comment