Na Sumai Salum- Kishapu
Balozi wa pamba Nchini Tanzania Mhe. Agrey Mwanri Leo Julai 15,2026 amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku mbili katika Vijiji Saba vya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga yenye lengo la kutoa elimu kwa wakulima kuhusu kilimo bora cha pamba kuanzia maandalizi ya mashamba hadi uvunaji unaozingatia kanuni na viwango vinavyotakiwa.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha ziara hiyo, Mhe. Mwanri, amesema lengo kuu ni kuhakikisha wakulima wanapata elimu sahihi kuhusu uzalishaji wa pamba wenye tija, matumizi sahihi ya pembejeo, utunzaji wa mashamba pamoja na uvunaji na uhifadhi wa pamba ili kuongeza ubora wa zao hilo na kipato cha mkulima.
"Niendelee kuwataka wananchi wote wa Kishapu ambao mmekuwa wakulima wazuri wa pamba basi tujitahidi msimu ujao tuhakikishe mnalima kwa kufuata taratibu zote Kumi za kilimo cha pamba" amesisitiza Mwanri
Hata hivyo mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Peter Masindi amempongeza balozi huyo kwa bidii anayoionesha ya kutekeleza maelekezo aliyopewa na Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuhakikisha wakulima wate wanafikiwa kwa maslahi Yao wenyewe.
"Na Mimi naungana na balozi wetu kuhimiza ulimaji sahihi wa zao la pamba ambalo ni kipaumbele cha Rais wetu ili wananchi wakulima waweze kunufaika na juhudi zao, wote mlioko hapa naombeni mkawe mabalozi wazuri na kuendelea kuwasaidia wengine kulima kwa wingi huku kanuni zote zikifuatwa' amesisitiza Mhe. Masindi
Mhe. Masindi amewatahadharisha wanaume katika msimu huu wa kuuza pamba wajitahidi kuwa na nidhamu ya fedha kwa kutunza na kuhudumia familia zao ambazo ndio muhimili wa mafanikio na kuachana na kuwafanyia wake zao na watoto ukatili mbalimbali ukiwemo wa kimaumbile na kihisia kwa sababu ya ulaghai wanaokutana nao mitaani kwa kujihusisha na mapenzi yasiyo rasmi na ulevi.
"Wako baadhi ya wanaume ambao wamekuwa na Tabia mbaya katika jamii kwani baada ya mavuno anasahahu kuwa pamba hiyo imelimwa na mke wake na watoto ambao wamesumbuka shambani lakini akienda kuuza anaishia kwenye vilabu vya pombe na kuanziaha mahusiano mapya na hata wanaporudi majumbani wanawapiga na kuwatukana wake zao hiyo ni laana acheni mara moja Tabia hiyo" amesisitiza Masindi
Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wakulima kuondokana na Tabia ya kukaa na pamba ndani kwani ni hatari pindi moto uwakapo hivyo wanapovuna wapeleke stoo kuuza kwani ndio eneo lililotemgwa maalumu kwa uhifadhi wake . Huku akiwataka watendaji wa Kata na Afisa Tarafa kuhakikisha Kila shamba la pambalililovunwa kwa zaidi ya wiki nne kuhakikisha mkulima anachoma moto ili kujiandaa na msimu ujao.
Nao baadhi ya wananchi wamepongeza jitihada hizo zinazooneshwa na serikali za kuwafikia mara kwa mara ili kuwapa elimu ya kujikwamua kiuchumi huku wakiahidi kubadilika na kuachana na ulimaji mseto wa zao la pamba na uvunaji usiozingatia kanuni.
Ziara hiyo ya siku mbili Julai 14,2026 imefanyika katika Vijiji vya Bulima, Bubiki, Bunambiyu na Itongoitale huku leo Julai 15, 2026, imeendelea katika vijiji vya Kishapu, Mwamashele, Mwamadulu na Masanga ambapo wakulima wamepatiwa mafunzo kuhusu maandalizi ya mashamba, usafi wa mashamba ya pamba, udhibiti wa magugu na wadudu pamoja na mbinu bora za uvunaji na uhifadhi wa pamba huku ziara hiyo ikiendelea kuonesha dhamira ya dhati ya serikali na wakulima kuunga mkono jitihada hizo kwa maendeleo endelevu.
Bonyeza hapa kusoma zaidi
https://www.sumai.co.tz/2026/07/zao-la-pamba-lawatoa-ofisini-balozi-wa.html
Balozi wa pamba nchini Tanzania Mhe. Agrey Mwanri akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wenye lengo la kutoa elimu kwa wakulima kuhusu kilimo bora cha pamba kuanzia maandalizi ya mashamba hadi uvunaji unaozingatia kanuni na viwango vinavyotakiwa ikiwa ni mwisho wa ziara yake ya siku mbili iliyomalizika leo Julai 5,2026 wilayani Kishapu mkoani Shinyanga
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi akizungumza kwenye ziara ya Balozi wa pamba nchini Tanzania Mhe. Agrey Mwanri yenye lengo la kutoa elimu kwa wakulima kuhusu kilimo bora cha pamba kuanzia maandalizi ya mashamba hadi uvunaji unaozingatia kanuni na viwango vinavyotakiwa ikiwa ni siku ya pili na ya mwisho ya ziara yake ya siku mbili Julai 15,2026 wilayani humo
Post a Comment