Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga imeendelea kuwa na hali ya amani, utulivu na usalama, huku juhudi za pamoja za Serikali na viongozi katika ngazi mbalimbali zikifanikiwa kumaliza mgogoro uliokuwa ukiendelea katika maeneobalimbali ya Wilaya hiyo, Aidha wastani wa kesi na matukio yanayoripotiwa kwa mwezi katika vituo vyote vya polisi wilayani humo umeendelea kuwa 74.Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Peter Nicholaus Masindi , wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025–2030 kwa kipindi cha Januari-Juni 2026 katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Siasa ya CCM Wilaya ya Kishapu, kilichofanyika leo Agosti 7, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa CCM Wilaya.
Katika taarifa hiyo, Mhe. Masindi amesema katika kipindi cha Januari hadi Juni 2026, Wilaya ya Kishapu ilipokea jumla ya Shilingi bilioni 5.2 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta za afya, elimu, kilimo, umeme, maji, barabara, sekta binafsi, viwanda na uwekezaji.
Kati ya fedha hizo, zaidi ya Shilingi bilioni 3.6 zilitumika katika shughuli na miradi iliyokuwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Akieleza kuhusu maendeleo ya jamii na uwezeshaji wa wananchi, Mkuu huyo wa Wilaya amesema jumla ya Shilingi milioni 486.3 zilitolewa kama mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, huku wafanyabiashara wadogo 176 wakitambuliwa na kupewa vitambulisho vya wajasiriamali wadogo.
Mhe. Masindi amesema Sekta ya Kilimo Wilaya ilipima sampuli 630 za udongo katika kata 24, kuhamasisha kilimo cha pamba katika ekari 214,232, kusajili wakulima 26,593 kwenye mfumo wa mbolea ya ruzuku na kusambaza tani 2,555 za mbegu za pamba pamoja na viuatilifu kwa wakulima 52,000 katika vijiji 117. Aidha, zana mbalimbali za kilimo zilitolewa ili kuongeza tija kwa wakulima.
Kuhusu umeme, elimu, afya na maji, taarifa hiyo imeeleza kuwa vitongoji 128 vilifanyiwa upembuzi yakinifu na kuanza kuunganishiwa umeme, huku jumla ya vitongoji 428 kati ya 614, sawa na asilimia 69, vikifikikiwa na huduma ya umeme. Kwa upande wa elimu, zaidi ya Shilingi bilioni 1.5 zilipokelewa, huku fedha zikitumika katika mitihani, ujenzi wa miundombinu ya shule na kuboresha mazingira ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
Katika sekta ya afya, Wilaya ilipokea zaidi ya Shilingi milioni 872.9, ambapo zaidi ya Shilingi milioni 728.7 zilitumika katika shughuli za maendeleo, ikiwemo afua za lishe, ujenzi wa miundombinu katika vituo vya afya na udhibiti wa TB, HIV na Malaria. Wakati huo huo, huduma ya maji iliongezeka na kufikia kaya 43,277 kutoka kaya 42,401, huku uzalishaji wa maji ukifikia lita milioni 7.9 kwa siku.
Kwa upande wa miundombinu ya barabara, matengenezo ya kawaida na maalum, maeneo korofi pamoja na ujenzi wa makalavati yamefanyika katika barabara zinazounganisha maeneo mbalimbali ikiwemo Mwadui–Lohumbo, Mondo, Sekebugoro, Maganzo, Idukilo, Bunambiyu, Busangwa na Songwa, kwa kutumia Shilingi milioni 456.2 kutoka Mfuko wa Bodi ya Barabara.
Aidha, taarifa hiyo imeonesha hatua zilizopigwa katika viwanda na uwekezaji, ambapo wawekezaji wawili wamekaribishwa, wakiwemo mwekezaji wa kituo cha mafuta na kiwanda cha kusindika alizeti, huku maeneo ya uwekezaji wa viwanda vidogo yakitengwa Isoso na Lubaga.











Post a Comment