DED JOHNSON AWAAGA WATUMISHI KISHAPU, AWATAKA KUENDELEZA UMOJA NA UTENDAJI KAZI

Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Emmanuel Johnson na sasa anaenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wanging'ombe mkoani Njombe akizungumza Septemba 30, 2026 wakati akiwaaga watumishi wa Halmashauri ya Kishapu
Aliyekuwa Afisa Tehama Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Jacobo Ngainayo aliyetumia nafasi hiyo pia kuwaaga watumishi wenzake baada ya kuhamishiwa Manisipaa ya Singida mkoani Singida

Na Sumai Salum-Kishapu

Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Emmanuel Johnson, amewataka watumishi wa Halmashauri hiyo kuendelea kushirikiana, kuheshimiana na kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma.


Johnson ameyasema hayo leo, Septemba 30, 2026, wakati akiwaaga watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, kufuatia uteuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, wa Septemba 29, 2026, uliomhamisha na kumteua kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe.


Amesema katika kipindi alichohudumu Kishapu, amejifunza mambo mengi kutoka kwa watumishi wenzake na kwamba mafanikio yaliyopatikana katika Halmashauri hiyo  kwa takribani miaka 6 hayakuwa ya mtu mmoja, bali ni matokeo ya ushirikiano, kujituma na uwajibikaji wa kila mtumishi, kuanzia viongozi hadi watumishi waliopo katika ngazi za chini.


“Ninawashukuru sana kwa ushirikiano wenu. Kila mmoja wenu ana nafasi kubwa katika mafanikio ya Halmashauri hii. Kuna wakati huenda juhudi za mtumishi wa chini zisionekane kwa urahisi, lakini kazi mnayoifanya kila siku ndiyo inayofanya Halmashauri iweze kutoa huduma kwa wananchi. Nawapongeza na kuwashukuru kwa moyo wangu wote, "amesema Johnson.


Aidha, Johnson amewataka watumishi kuendelea kuwa timu moja, kusaidiana na kuepuka migawanyiko, akisisitiza kuwa tofauti za kiutendaji zinapaswa kutatuliwa kwa mazungumzo, kuheshimiana na kuzingatia taratibu za utumishi.


Amewataka pia watumishi kumpa ushirikiano wa kutosha Mkurugenzi Mtendaji atakayekuja, akieleza kuwa mabadiliko ya viongozi ni sehemu ya utumishi wa umma na kwamba kinachopaswa kuendelea kuwa imara ni taasisi na huduma kwa wananchi.


“Mimi nimefika Kishapu, nimefanya sehemu yangu, na sasa nimepewa jukumu jingine. Naondoka nikiwa na heshima na shukrani kubwa kwenu. Nawaomba msimame pamoja, mumsaidie atakayekuja na muendelee kuwatumikia wananchi kwa moyo ule ule. Kila mmoja aendelee kufanya kazi yake kwa uadilifu, nidhamu na uzalendo, "amesema.


Johnson pia amewataka watumishi kutambua kuwa nafasi walizonazo ni dhamana ya kuihudumia jamii, hivyo wanapaswa kuzitumia kwa kuleta matokeo chanya na kuhakikisha huduma zinazotolewa na Halmashauri zinaendelea kuboreshwa.


Kwa upande mwingine, amewashukuru watumishi kwa uvumilivu, ushauri na ushirikiano waliompa wakati wa uongozi wake, akisema mambo aliyofanikiwa kuyatekeleza Kishapu yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na nguvu ya pamoja ya watumishi.


“Kama kuna mahali nilikosea, naomba mnielewe kwa sababu nilikuwa binadamu. Na kama kuna jambo nililofanya likamgusa au kumsaidia mmoja wenu, basi hilo ndilo jambo nitakalolibeba moyoni. Nawaachia Kishapu si kwa maana ya kuwa nimeondoka katika moyo, bali naondoka nikiwa nimeacha ndugu na marafiki wengi, "amesema Johnson".


Hatua hiyo imekuja baada ya uteuzi uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Septemba 29, 2026, ambapo Johnson amehamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu na kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe huku Kishapu akiteuliwa kuingoza Niceferus Martin Mgaya. 

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم