MKUTANO WA 46 WA WAKUU WA MAMLAKA ZA KODI ZA JUMUIYA YA MADOLA KUFUNGUIWA NA MAKAMO WA RAIS

Na Bora Mustafa Arusha.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa Mkutano wa 46 wa Chama cha Wasimamizi wa Kodi cha Jumuiya ya Madola (CATA), utakaofanyika jijini Arusha na kuwakutanisha viongozi na wataalamu zaidi ya 400 kutoka mataifa 48.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano, Septemba 30, 2026, Ofisini kwake jijini Arusha, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla, amesema Tanzania imepata heshima ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo kwa mara ya kwanza, akieleza kuwa ni fursa muhimu kwa nchi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).


Amesema mkutano huo wenye kaulimbiu “Matumizi ya Teknolojia katika Kuboresha Ufanisi wa Ukusanyaji wa Mapato” utatoa nafasi kwa TRA kubadilishana uzoefu na mamlaka nyingine za kodi, kujenga uwezo wa wataalamu wake na kujifunza mifumo na teknolojia zinazoweza kuboresha usimamizi wa kodi na huduma kwa walipa kodi.


Pia Mhe. Makalla amesema kuwa, pamoja na masuala ya kodi, Arusha na Tanzania itanufaika na fursa ya kuonesha uwezo wake wa kuwa mwenyeji wa mikutano mikubwa ya kimataifa, huku wajumbe kutoka mataifa 48 wakipata nafasi ya kutambua vivutio vya utalii vya nchi, ikiwemo Serengeti, Mlima Kilimanjaro na Ngorongoro.


Aidha amesema uwepo wa mkutano huo jijini Arusha pia unatarajiwa kuchochea shughuli za kiuchumi kupitia sekta za hoteli, usafirishaji, huduma za mikutano na biashara nyingine zinazohusiana na utalii, huku akiwataka wananchi kuchangamkia fursa za kiuchumi katika Mkutano huo na kuwa mabalozi wazuri wa ukarimu na utoaji wa huduma bora kwa wahudhuriaji wa Mkutano huo.

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم