Kaimu Afisa Tawala wa mkoani Mwanza, Daniel Machunda ambaye pia alikuwa Mwakilishi wa Mgeni rasmi katika kongamano hilo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. CP Salum Hamduni, akizungumza kwenye kongamano la MISA TAN na Taasisi za umma na binafsi kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi Kisekta kupitia Uandishi wa Habari lililoanza leo Oktoba 12 hadi 13,2026 katika ukumbi wa mikutano Benki kuu ya Tanzania Jijini Mwanza
Na Sumai Salum-Shinyanga
Shirika la Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, tawi la Tanzania (MISA-TAN), limewakutanisha wanahabari na wadau kutoka taasisi za umma na binafsi katika kongamano linalolenga kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari kiuchumi, kuongeza weledi wa waandishi na kukuza mchango wa sekta ya habari katika maendeleo ya uchumi wa taifa.
Kongamano hilo limeanza Oktoba 12 na linatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 13, 2026, katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Mwanza, likiwa na kaulimbiu ya “Uhuru wa Vyombo vya Habari Kiuchumi.” Mgeni rasmi katika kongamano hilo ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. CP Salum Hamduni, aliyewakilishwa na Kaimu Afisa Tawala wa Mkoa huo, Daniel Machunda.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Machunda ameipongeza MISA-TAN pamoja na wanahabari kwa jitihada na weledi wanaouonesha katika kutekeleza majukumu yao, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha taaluma ya habari na mchango wake katika kuhabarisha jamii na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Amesema vyombo vya habari ni injini muhimu ya kuchochea ukuaji wa uchumi duniani, kwa kuwa vina nafasi kubwa ya kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu utendaji wa taasisi za umma na binafsi, mafanikio yaliyopatikana, miradi inayotekelezwa na fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini. Ameeleza kuwa kupitia taarifa sahihi na zenye tija, wananchi wanaweza kufahamu kinachoendelea katika maeneo yao na kutambua manufaa ya miradi hiyo katika kuboresha maisha yao na kukuza uchumi wa taifa.
Aidha, amezitaka taasisi za umma na binafsi kuimarisha ushirikiano na wanahabari kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu miradi, huduma, fursa za uwekezaji na mafanikio yao, ili jamii iweze kufahamu kwani ushirikiano huo utasaidia kuongeza uwazi na uwajibikaji, kutangaza fursa za kiuchumi na kuhakikisha taarifa zenye manufaa kwa umma zinawafikia wananchi kwa wakati.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa MISA-TAN, Edwin Soko, amesema kongamano hilo ni fursa muhimu kwa wanahabari kubadilishana uzoefu, kujengeana uwezo na kuboresha viwango vya uandishi wa habari. Amesisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili, usahihi na weledi katika kazi zao ili kulinda hadhi ya taaluma ya habari na kuitofautisha na uandishi usiozingatia misingi ya kitaaluma.
Soko amebainisha pia umuhimu wa kuimarisha mazingira ya kiuchumi ya vyombo vya habari ili viweze kujiendesha kwa ufanisi, kulinda uhuru wa uhariri na kutekeleza wajibu wao wa kuhabarisha umma kwa kuzingatia misingi ya taaluma.
Kongamano hilo limewapa wanahabari fursa ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujenga mawasiliano na wadau mbalimbali kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi na kuimarisha ushirikiano kati ya vyombo vya habari na taasisi zinazotoa huduma kwa umma.
Taasisi na wadau walioshiriki kongamano hilo ni pamoja na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), TASHICO, Idara ya Uhamiaji, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Bima ya Afya kwa Wote, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Mwenyekiti wa MISA-TAN, Edwin Soko akizungumza kwenye kongamano la MISA TAN na Taasisi za umma na binafsi kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi Kisekta kupitia Uandishi wa Habari lililoanza leo Oktoba 12 hadi 13,2026 katika ukumbi wa mikutano Benki kuu ya Tanzania Jijini Mwanza 










Tazama picha za Kongamano hapa👇





إرسال تعليق