Na Sumai Salum – Kishapu
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Josephat Limbe, amefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji Cha Butuyu Kata ya Bunambiyu wilayani humo kwa lengo la kusikiliza na kutafuta ufumbuzi wa kero zinazowakabili katika sekta ya afya, akisisitiza umuhimu wa kuboresha utoaji wa huduma na kuhakikisha Wananchi wanapata huduma zinazostahili kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo ya Serikali.
Katika mkutano huo uliofanyika Oktoba 16,2026 katika Kituo cha Afya Bunambiyu, wananchi wewasilisha malalamiko yanayohusu gharama za baadhi ya dawa na huduma, utaratibu wa malipo kupitia namba za malipo (Control Number), pamoja na madai ya kutoridhishwa na namna baadhi ya watumishi wanavyowapokea na kuwahudumia wanapofika katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Mhe. Limbe ameeleza kuwa malalamiko ya wananchi yanapaswa kusikilizwa na kufanyiwa kazi kwa kufuata taratibu zilizowekwa, huku akisisitiza umuhimu wa watumishi kuwajibika na kutekeleza majukumu yao kwa weledi, heshima na kuzingatia haki za wananchi wanaohitaji huduma za afya.
Limbe ameongeza kuwa mkutano huo ni fursa ya kujadiliana na wananchi kuhusu changamoto zinazowakabili, kupata ufafanuzi kutoka kwa wataalamu na kuweka msingi wa hatua zitakazosaidia kuboresha huduma. Alisisitiza pia umuhimu wa wananchi kuelewa taratibu za kupata huduma na kutumia njia rasmi kuwasilisha malalamiko ili yaweze kufanyiwa kazi na mamlaka husika.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Dkt. Joseph Bahati, amefafanua kuhusu huduma za afya zinazotolewa kwa wajawazito, hususan wanapohudhuria kliniki kwa mara ya kwanza kwa ajili ya uchunguzi wa kina kwa mjamzito anapohudhuria kwa mara ya kwanza( idhurio la kwanza), matibabu kwa Watoto, Wazee na Wagonjwa wengine kwa kuzingatia miongozo rasmi ya Serikali kwenye misamaha ya malipo na huduma zinazopaswa kutolewa malipo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Josephat Limbe, amefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji Cha Butuyu Kata ya Bunambiyu wilayani humo kwa lengo la kusikiliza na kutafuta ufumbuzi wa kero zinazowakabili katika sekta ya afya Oktoba 16,2026
Ameongeza kuwa ni umuhimu wa wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu huduma zinazotolewa katika vituo vya afya, gharama zinazohusika na taratibu za kufuata, ili kuepusha mkanganyiko na kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi wanapohitaji matibabu.
Mwakilishi wa Afisa Utumishi wa Halmashauri hiyo, Hamadi Kisema, amezungumzia umuhimu wa watumishi wa umma kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya utumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu yao. Ameeleza kuwa watumishi wanapaswa kuzingatia maadili ya kazi, kuwahudumia wananchi kwa heshima na kutoa maelezo yanayoeleweka kuhusu huduma wanazohitaji. Aidha, malalamiko yanayohusu mwenendo wa watumishi yanapaswa kuwasilishwa kwa mamlaka husika ili yafanyiwe uchunguzi na kushughulikiwa kwa mujibu wa taratibu zilizopo kwa haraka zaidi.
Diwani wa Kata ya Bunambiyu kwa tiketi ya chama cha ACT Wazalendo Mhe. Adrian Zengo amesema ofisi yake imewahi kupokea malalamiko yanayofanana na hayo yaliyowasilishwa katika mkutano huo, akieleza kuwa changamoto hizo zimekuwa miongoni mwa hoja zinazohitaji ufuatiliaji ili wananchi wapate huduma bora.
Ameongeza kuwa bado ana matumaini kuwa mazungumzo yaliyofanyika na ufafanuzi uliotolewa na viongozi pamoja na wataalamu utasaidia kupunguza na hatimaye kuondoa changamoto hizo, huku akitarajia kuwa hatua stahiki zitachukuliwa ili kuboresha mahusiano kati ya wananchi na watoa huduma za afya.
Kwa upande wao, wananchi waliomba changamoto walizozieleza zifanyiwe kazi, wakisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa uwazi kuhusu gharama za huduma, utaratibu wa malipo na kuboreshwa kwa namna wanavyopokelewa na kuhudumiwa katika vituo vya afya.
Hatua ya Mwenyekiti wa Halmashauri kukutana na wananchi na kusikiliza kero zao ni fursa muhimu ya kuimarisha uwajibikaji na kuboresha huduma za afya. Hata hivyo, mafanikio ya mkutano huo yatapimwa zaidi kwa hatua zitakazochukuliwa baada ya malalamiko hayo kuwasilishwa, ikiwemo kufuatilia utekelezaji wa maelekezo, kutoa mrejesho kwa wananchi na kuhakikisha changamoto zilizobainika zinapatiwa ufumbuzi.
Ni muhimu pia Halmashauri kuendelea kutoa elimu ya afya kwa wananchi kuhusu haki zao, huduma zinazopaswa kutolewa bila malipo, huduma zenye gharama, utaratibu rasmi wa malipo na njia za kuwasilisha malalamiko. Uwazi katika kuweka na kueleza gharama za huduma utasaidia kupunguza mkanganyiko na kujenga imani kati ya wananchi na watoa huduma.
Vilevile, wananchi wanapaswa kuhamasishwa kuhusu umuhimu wa kuwa na Bima ya Afya kwa Wote na mifumo ya bima inayotambulika, kwani inaweza kusaidia kupunguza mzigo wa gharama za matibabu na kuwezesha kaya kupata huduma kwa wakati huku wakikubali kubadilika kutokana na sera zinazotolewa na serikali na kudumisha mahusiano mazuri na watalamu kwenye maeneo yao.
Kwa upande wa watumishi wa afya, ni muhimu kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, kutoa huduma kwa heshima na huruma, na kuhakikisha kila mwananchi anapata maelezo sahihi kuhusu huduma anazohitaji. Ushirikiano kati ya viongozi, wataalamu wa afya na wananchi ni msingi muhimu wa kujenga mfumo wa huduma za afya wenye uwazi, uwajibikaji na unaozingatia mahitaji ya wananchi.
Diwani wa Kata ya Bunambiyu wilayani Kishapu mkoani Shinyanga kwa tiketi ya chama cha ACT Wazalendo Mhe. Adrian Zengo akizungumza kwenye mkutano huo wa mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Josephati Limbe wa kusikiliza na kutoa ufafanuzi wa kero wanazokutana nazo wananchi katika sekta ya afya Oktoba 16,2026
Mwenyekiti wa Kijiji cha Butuyu Kata ya Bunambiyu wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga, Masaba Basu akizungumza wakati akifungua mkutano huo
إرسال تعليق