WANACHAMA WA MISA TANZANIA WATEMBELEA DARAJA LA MAGUFULI NA MELI YA MV NEW MWANZA

Mwenyekiti wa MISA Tanzania - Edwin Soko akizungumza Wanachama wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA Tanzania) katika Daraja la John Pombe Magufuli (Kigongo–Busisi).Picha na Kadama Malunde
Wanachama wa MISA TAN wakiwa katika Daraja la John Pombe Magufuli (Kigongo–Busisi) jijini Mwanza. 
Wanachama wa MISA TAN wakiwa katika Daraja la John Pombe Magufuli (Kigongo–Busisi) jijini Mwanza.
Wanachama wa MISA TAN wakiwa katika mradi wa ujenzi wa meli kubwa ya kisasa ya MV New Mwanza katika Bandari ya Mwanza.
Wanachama wa MISA Tanzania wakipata maelezo kuhusu mradi wa ujenzi wa meli kubwa ya kisasa ya MV New Mwanza walipotembelea Bandari ya Mwanza, Oktoba 13, 2026.
Wanachama wa MISA Tanzania wakipata maelezo kuhusu mradi wa ujenzi wa meli kubwa ya kisasa ya MV New Mwanza walipotembelea Bandari ya Mwanza, Oktoba 13, 2026.

Wanachama wa MISA TAN wakiwa katika mradi wa ujenzi wa meli kubwa ya kisasa ya MV New Mwanza katika Bandari ya Mwanza.




Na Kadama Malunde – Malunde 1 Blog

Wanachama wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA Tanzania), wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Edwin Soko, wametembelea miradi ya kimkakati ya Serikali jijini Mwanza, ikiwemo ujenzi wa meli ya kisasa ya MV New Mwanza na Daraja la John Pombe Magufuli (Kigongo–Busisi), ili kujionea maendeleo yake na kuelewa mchango wake katika kukuza uchumi wa Taifa.

Ziara hiyo imefanyika Oktoba 13, 2026, siku moja baada ya kongamano la wadau wa habari kutoka taasisi za umma na sekta binafsi lililofanyika jijini Mwanza, Oktoba 12, 2026, kujadili namna vyombo vya habari vinavyoweza kuchochea ukuaji wa uchumi, likiwa na kaulimbiu “Uhuru wa Vyombo vya Habari Kiuchumi.”
Kongamano hilo lilishirikisha wanachama 60 wa MISA Tanzania kutoka Kanda ya Ziwa, inayojumuisha mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Geita, Simiyu, Mara na Kagera; Kanda ya Magharibi inayojumuisha Kigoma, Tabora na Katavi, pamoja na Kanda ya Kati inayojumuisha Singida na Dodoma, wakikutana na wadau mbalimbali kutoka taasisi za umma na sekta binafsi.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Soko ameipongeza Serikali kwa kuwekeza katika miradi hiyo mikubwa, akisema ina nafasi muhimu katika kuboresha usafiri na usafirishaji na kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi.

“Kwanza tumefurahishwa sana kuona mamlaka za nchi zinawekeza kwenye miradi mikubwa na ya kimkakati kama hii meli na daraja ndani ya Ziwa Victoria,” amesema Soko.

Ameiomba Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuendelea kutumia vyombo vya habari kutangaza miradi ya maendeleo ili wananchi wafahamu uwekezaji unaofanyika na manufaa yake kwa jamii.

“Ninaiomba Serikali ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan itumie waandishi wa habari kutangaza miradi ya maendeleo ili jamii ifahamu zaidi,” amesema.
Kwa upande wake, Afisa Uhusiano wa Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO), Abdulrahman Ally, amesema meli ya MV New Mwanza inatarajiwa kuimarisha usafiri kati ya Mwanza na Bukoba mkoani Kagera, ikiwa na uwezo wa kubeba tani 400 za mizigo na abiria 1,200 kwa safari moja.

Amesema meli hiyo imezingatia pia mahitaji ya kijamii, ikiwemo uwepo wa lifti kwa ajili ya watu wenye ulemavu, pamoja na huduma zinazozingatia mahitaji ya wajawazito na wagonjwa.
Nalo Daraja la John Pombe Magufuli, linalounganisha Kigongo na Busisi, ni sehemu muhimu ya miundombinu ya usafiri katika Ukanda wa Ziwa Victoria, likilenga kurahisisha safari, kupunguza utegemezi wa vivuko na kuboresha usafirishaji wa bidhaa na huduma.

Kupitia ziara hiyo, wanahabari wamepata fursa ya kujifunza kuhusu miradi hiyo na nafasi ya uandishi wa habari katika kuelimisha umma kuhusu uwekezaji, maendeleo ya miundombinu na fursa za kiuchumi zinazoweza kunufaisha wananchi.

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم