Mkoa wa Shinyanga umeendelea kuonesha dhamira thabiti katika kulinda afya za watoto baada ya kupokea ugeni kutoka Wizara ya Afya uliolenga kukagua na kujiridhisha na maandalizi ya kampeni ya chanjo ya polio awamu ya pili itakayoanza Mei 7-10, 2026 kwa watoto wenye umri chini ya miaka 10.
Ugeni huo umeongozwa na Mkurugenzi wa Kinga, Dkt. Otia Gowele, ambaye amefanya kikao na Katibu Tawala wa Mkoa, CP Salum Hamduni, pamoja na Timu ya Usimamizi ya Afya Mkoa (RHMT) ili kupata tathmini ya kina ya hatua zilizofikiwa kuelekea utekelezaji wa kampeni hiyo muhimu.
Akizungumza katika kikao hicho,Katibu Tawala Mkoani humo, CP Salum Hamduni ameeleza kufurahishwa na ujio wa ujumbe huo, akisisitiza kuwa Mkoa wa Shinyanga umejipanga kikamilifu kuhakikisha kampeni hiyo inafikia malengo yaliyokusudiwa. Alibainisha kuwa mifumo ya usimamizi imeimarishwa kuanzia ngazi ya mkoa hadi wilaya na vituo vya huduma za afya, jambo linalotoa uhakika wa utekelezaji wenye ufanisi.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa, Bw. Timothy Sosoma, alisema maandalizi yamekamilika kwa kiwango cha kuridhisha, huku halmashauri zote zikiwa tayari zimepokea vifaa muhimu kwa ajili ya utoaji wa chanjo ya polio.
Sosoma amesema Shinyanga ipo tayari kutekeleza kampeni hiyo, huku akibainisha kuwa Halmashauri zote tayari zimepokea vifaa muhimu vinavyohitajika kwa ajili ya utoaji wa chanjo ya polio awamu ya pili.
Naye Mratibu wa Elimu ya Afya Mkoa, Moses Mwita, alieleza kuwa juhudi kubwa zimefanyika katika utoaji wa elimu kwa umma, ambapo wananchi wameendelea kuhamasishwa kupitia njia mbalimbali ikiwemo vituo vya kutolea huduma za afya, ili kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kuwapeleka watoto kupata chanjo.
Akihitimisha ziara hiyo, Dkt. Gowele alizitaka timu za afya katika ngazi zote kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa chanjo hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa kufanya tathmini ya kila siku wakati wa kampeni ili kubaini changamoto na kuzitatua kwa wakati.
Kampeni ya chanjo ya polio awamu ya pili ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuhakikisha ugonjwa huo unatokomezwa kabisa, huku ushirikiano wa wananchi ukiendelea kuwa nguzo muhimu ya mafanikio yake.






إرسال تعليق