Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limepongezwa kwa ushirikiano wake na waandaaji pamoja na wananchi katika kuhakikisha amani, usalama na ulinzi wa raia na mali zao vinadumishwa wakati wote wa mashindano ya soka ya DINDAI CUP 2026.Pongezi hizo zimetolewa na mratibu wa mashindano hayo, Moshi Ramadhani, amesema mashindano hayo yalianza Juni 1, 2026 na kuhitimishwa Juni 26, 2026 katika Uwanja wa Pepsi, uliopo Kata ya Chamaguha, Manispaa ya Shinyanga. Alisema jumla ya timu nane zilishiriki, ikiwemo timu ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga maarufu C-COY FC.
Ramadhani amesema Jeshi la Polisi limetoa ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha mashindano yanafanyika katika mazingira ya amani na utulivu. Alieleza kuwa kila pale kulipojitokeza viashiria vya uvunjifu wa amani au sintofahamu miongoni mwa mashabiki, askari walifika kwa wakati na kudhibiti hali hiyo kwa weledi, jambo lililochangia mashindano hayo kumalizika salama bila matukio makubwa ya kiusalama.
Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Fraterine Tesha, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mchezo wa fainali, aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kudumisha amani na usalama.
Akizungumza na vijana na wadau wa michezo, ACP Tesha amesema vijana wana nafasi kubwa katika kulinda amani ya jamii kwa kuzingatia sheria, kuepuka vitendo vya uhalifu na kutoa taarifa kwa vyombo vya dola pale wanapoona viashiria vya uhalifu.
"Nyinyi vijana mna mchango mkubwa katika kulinda amani na utulivu wa nchi yetu. Endeleeni kushiriki kikamilifu katika ulinzi shirikishi, kutoa taarifa za uhalifu kwa wakati na kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuhakikisha jamii inaendelea kuwa salama," amesema ACP Tesha.
Katika mchezo wa fainali wa mashindano hayo, timu ya Chipukizi FC iliibuka bingwa baada ya kuifunga Chamaguha FC bao 1-0 lililofungwa kwa njia ya mkwaju wa penalti. Kwa ushindi huo, Chipukizi FC ilitwaa ubingwa wa DINDAI CUP 2026, huku timu ya C-COY FC ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ikimaliza katika nafasi ya tatu.









إرسال تعليق