Mkuu wa wilaya ya Ukerewe Cde. Christopher Ngubiagai
Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani inaendelea kuzaa matunda, huku Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ikitekeleza kwa vitendo maelekezo hayo kwa kutoa mikopo yenye thamani ya Shilingi milioni 586.5 kwa vikundi 57 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Hatua hiyo inaakisi dhamira ya Serikali ya kuhakikisha makundi maalum yanapata fursa za kiuchumi, kujiongezea kipato, kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa taifa unaojumuisha wananchi wote.
Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji wa mikopo hiyo iliyofanyika Juni 10, 2026 katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Bukongo, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Christopher Ngubiagai, amesema utekelezaji wa mikopo hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Rais Samia za kuwainua wananchi kiuchumi na kuharakisha maendeleo katika ngazi ya wilaya.
Amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki yanayowezesha wananchi kupata mitaji kwa masharti nafuu ili waweze kuanzisha na kukuza shughuli za uzalishaji mali, hatua inayochochea ukuaji wa uchumi wa kaya na jamii kwa ujumla.
"Serikali ya Rais Samia imeweka mkazo mkubwa katika uwezeshaji wa wananchi kiuchumi. Sisi kama wasimamizi wa Serikali katika ngazi ya wilaya tuna wajibu wa kuhakikisha fursa hizi zinawafikia walengwa na kuleta matokeo chanya katika maisha yao," amesema Ngubiagai.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Vicent Mbua, amesema jumla ya Shilingi milioni 586.5 zimetolewa kwa vikundi 57 vilivyokidhi vigezo vya kupata mikopo hiyo.
Amefafanua kuwa awali vikundi 90 viliwasilisha maombi ya mikopo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 2.4, hali inayoonesha mwitikio mkubwa wa wananchi katika kutumia fursa zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.
Mbua amesema kati ya vikundi hivyo, vikundi 48 vilinufaika katika awamu ya pili kwa kupatiwa Shilingi milioni 444.2, huku vikundi vingine tisa vikipatiwa Shilingi milioni 142.3, na hivyo kufanya jumla ya vikundi 57 kunufaika na mpango huo.
Aidha, amesema halmashauri itaendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuongeza kiwango cha fedha kinachotengwa kwa ajili ya mikopo hiyo, hatua itakayowezesha wananchi wengi zaidi kunufaika na fursa za kiuchumi zinazotolewa na Serikali.
Katika kuonesha dhamira ya kutomuacha mwananchi nyuma, vikundi 33 vilivyobainika kuwa na upungufu wa baadhi ya taarifa vimeshauriwa kufanya maboresho yanayohitajika ili viweze kunufaika katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027 unaoanza Julai Mosi.
Mbua pia ameeleza kuwa Serikali itaendelea kutoa elimu na hamasa katika kata ambazo bado hazijawasilisha maombi ya mikopo, ikiwemo Igalla, Mukituntu, Bukiko, Nyamanga, Bwisya na Irugwa, ili wananchi wa maeneo hayo nao waweze kushiriki kikamilifu katika fursa hizo za maendeleo.
Naye Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri hiyo, Wanchoke Chinchibela, amesema idara yake itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mpango huo ili kuhakikisha fedha zinazotolewa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na marejesho yanafanyika kwa wakati.
Amesema usimamizi huo utasaidia fedha hizo kuendelea kuwafikia wananchi wengine wengi zaidi, sambamba na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii.
Utoaji wa mikopo hiyo unaendelea kuthibitisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kusogeza maendeleo karibu na wananchi kwa kuwapatia fursa za kiuchumi zinazowawezesha kushiriki kikamilifu katika safari ya kujenga Tanzania yenye uchumi imara na jumuishi.





إرسال تعليق