
Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Baada ya kuwafikia zaidi ya wananchi milioni nne wa Tanzania Bara katika Awamu ya Kwanza, Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia sasa inaingia Zanzibar ikiwa na lengo la kupanua huduma za haki kwa wananchi wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali za kisheria ikiwemo migogoro ya talaka, mirathi, ukatili wa kijinsia na madai ya kiraia.
Awamu ya Pili ya kampeni hiyo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan Juni 20, 2026 katika Viwanja vya Dole, Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha wananchi wote wanapata haki kwa wakati kupitia huduma za msaada wa kisheria.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Juni 17, 2026 kuhusu maandalizi ya uzinduzi huo, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera, alisema kampeni hiyo ni utekelezaji wa maono ya Rais Samia ya kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati bila vikwazo vya ukosefu wa uelewa wa sheria au gharama za huduma za kisheria.
Amesema kampeni hiyo inashughulikia masuala mbalimbali yanayowagusa wananchi katika maisha yao ya kila siku ikiwemo madai ya kiraia, migogoro ya ardhi, mirathi, talaka, ndoa, haki za watoto, haki za wafanyakazi, ukatili wa kijinsia, uhalifu wa mtandao, pamoja na masuala ya elimu na rushwa.
Dkt. Homera amesema programu hiyo imepewa jina la Rais Samia kutokana na nafasi yake ya kuimarisha upatikanaji wa haki nchini, hasa kwa wananchi wanaokosa huduma za kisheria kutokana na kutofahamu sheria au kushindwa kumudu gharama za uwakilishi wa kisheria.
"Rais Samia alibaini kuwa wananchi wengi walikuwa wanakosa haki zao kwa sababu hawazifahamu sheria, huku wengine wakichelewa kupata haki kutokana na kukosekana kwa msaada wa kisheria. Ndipo akaagiza kuanzishwa kwa kampeni hii ili kuwafikia wananchi moja kwa moja," amesema.
Amesema mafanikio ya awamu ya kwanza yameonesha umuhimu wa kuendeleza kampeni hiyo, ambapo maelfu ya wananchi walipatiwa msaada wa kisheria na wengine kusaidiwa kupata mawakili waliowasimamia hadi haki zao zilipopatikana.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Rais Samia ameridhishwa na matokeo ya awamu ya kwanza na kuagiza huduma hizo ziongezwe Zanzibar ili kuhakikisha wananchi wa pande zote za Muungano wananufaika kwa usawa.
"Lengo letu ni kuhakikisha huduma za msaada wa kisheria zinawafikia Watanzania wote bila kujali wanaishi upande gani wa Muungano. Baada ya uzinduzi Zanzibar, huduma hizi zitaendelea kutolewa katika mikoa, wilaya na vijiji mbalimbali nchini," amesema.
Dkt. Homera amesema zaidi ya wananchi 20,000 wanatarajiwa kushiriki katika uzinduzi huo, huku timu za wataalamu wa sheria zikiwa tayari kutoa huduma za ushauri na msaada wa kisheria kwa wananchi.
Akizungumzia changamoto zinazowakabili wananchi, ametaja migogoro ya ndoa, talaka na ukatili wa kijinsia bado ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazogusa jamii.
Amesema baadhi ya wananchi wameendelea kuvumilia manyanyaso ndani ya familia kwa muda mrefu bila kutoa taarifa kwa mamlaka husika, hali inayochangia kuendelea kwa vitendo hivyo.
"Ukipigwa au ukinyanyaswa usikae kimya. Toa taarifa ili hatua zichukuliwe. Sio wanawake pekee wanaonyanyaswa, hata wanaume wanakumbana na changamoto hizo. Haki lazima ilindwe kwa mujibu wa sheria," alisema.
Aidha, alisema migogoro ya mirathi imeendelea kusababisha migawanyiko ndani ya familia nyingi kutokana na uelewa mdogo wa taratibu za kisheria.
Amesema kampeni hiyo itatoa elimu ya sheria, ushauri wa kisheria na msaada wa moja kwa moja kwa wananchi ili kuwasaidia kupata ufumbuzi wa changamoto hizo.
"Safari hii tunaenda kusambaza upendo katika jamii, kuwaelimisha wananchi na kuwapa tabasamu litakalosaidia kujenga jamii yenye amani, usawa na maendeleo," alisema.
Kuhusu haki za wafanyakazi, Dkt. Homera alisema Serikali imekuwa ikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wafanyakazi wanaodai stahiki zao kwa muda mrefu bila mafanikio.

Amesema wataalamu wa kampeni hiyo watafika katika taasisi na maeneo mbalimbali kusikiliza changamoto hizo na kusaidia upatikanaji wa haki kwa mujibu wa sheria.
Pia amesema wanafunzi ni miongoni mwa walengwa wa kampeni hiyo kutokana na baadhi yao kukumbana na changamoto za kinidhamu, upangaji wa kozi na masuala mengine yanayohitaji ushauri wa kisheria.
Katika hatua nyingine, alisema kampeni hiyo itatoa elimu kuhusu mapambano dhidi ya rushwa, uhalifu wa mtandao na matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro ili kupunguza uhitaji wa mashauri mahakamani.
Amefafanua kuwa jukumu la kampeni si kuchukua nafasi ya mahakama bali kutoa ushauri wa kisheria na kuwaelekeza wananchi namna sahihi ya kufuata taratibu za kisheria.
"Sisi si mahakama. Sisi ni washauri wa kisheria. Tunawasaidia wananchi kuelewa haki zao na namna ya kuzidai kwa mujibu wa sheria," amesema.
Aidha, timu za kampeni hiyo zinatarajiwa kufika hadi magerezani kusikiliza changamoto za wafungwa na mahabusu, wakiwemo wanaodai kubambikiziwa kesi au kukosa msaada wa kisheria.
Dkt. Homera amesema Awamu ya Pili ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ni hatua muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa haki na kupunguza kero za kisheria kwa wananchi.
Kaulimbiu ya kampeni hiyo ni "Msaada wa Kisheria kwa Haki, Amani na Maendeleo."
"Tunaamini popote penye haki na usawa kuna maendeleo. Sheria ni sehemu ya maisha ya kila siku ya kila Mtanzania, hivyo ni muhimu kila mmoja afahamu haki zake na kutimiza wajibu wake," alisema.

إرسال تعليق