DIWANI WA KATA YA MAGANZO AHIMIZA UWEKEZAJI NA AJIRA

Na Sumai Salum- Kishapu 

Diwani wa Kata ya Maganzo, Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Hamza Tandiko, amezindua rasmi miradi miwili ya maendeleo ambayo ni Maganzo Barbershop na Jenga na Sisi yenye thamani ya Tsh. Milioni 40 inayomilikiwa na mfanyabiashara kijana Najim Seif Salum.


Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Julai Mosi, 2026 Mhe. Tandiko amempongeza kijana huyo kwa kuchukua hatua ya kuwekeza katika miradi yenye tija badala ya kusubiri ajira. Amesema uwekezaji wa aina hiyo unachochea maendeleo ya uchumi wa eneo husika na kutoa fursa za ajira kwa wananchi, hususan vijana.


Diwani huyo amewataka Vijana wa Kata ya Maganzo kuiga mfano wa Najim kwa kuthubutu kuanzisha biashara na miradi inayoongeza thamani kwa jamii. Aidha, amemshauri mmiliki kuhakikisha eneo la biashara linakuwa sehemu ya utoaji wa huduma na shughuli za maendeleo, badala ya kuwa kijiwe cha mazungumzo yasiyo na tija au mikusanyiko isiyo rasmi ya vijana.


"Natamani kuona eneo hili linaheshimika kwa kazi, nidhamu na utoaji wa huduma bora kwa wananchi. Liwe sehemu ya kujifunza kazi, kujenga uchumi na kuwapa vijana matumaini ya kujiajiri, si sehemu ya kupoteza muda kwa mazungumzo yasiyo na manufaa," amesema Mhe. Hamza Tandiko.


Kwa upande wake, mmiliki wa miradi hiyo, Najim Seif Salum, amesema amewekeza zaidi ya shilingi milioni 40 katika mradi wa Maganzo Barbershop kwa lengo la kusogeza huduma za kisasa na zenye ubora karibu na wananchi wa Maganzo na maeneo jirani.


Najim ameongeza kuwa, malengo yake makuu ya kuanzisha miradi hiyo ni pamoja na Kutoa huduma bora na za kisasa kwa jamii,Kutengeneza ajira kwa vijana wa eneo la Maganzo, Kuchangia ukuaji wa uchumi wa jamii kupitia uwekezaji wa ndani, Kuonyesha kuwa vijana wanaweza kufanikiwa kupitia ubunifu, nidhamu na uwekezaji na Kuongeza fursa za biashara na huduma zinazokidhi mahitaji ya wananchi.


Amebainisha kuwa miradi hiyo itatoa ajira za moja kwa moja kwa wafanyakazi zaidi ya nane (8). 
Aidha, kupitia mradi WA jenga na sisi utakaojihusisha na shughuli za kilimo biashara, kampuni yake huajiri vijana watano huku pia ikitoa fursa kwa zaidi ya vibarua 30 kila wiki kushiriki katika shughuli mbalimbali za uzalishaji.


Najim amewashukuru viongozi wa serikali na wananchi wa Maganzo kwa ushirikiano wao, akiahidi kuendelea kuwekeza katika miradi yenye manufaa kwa jamii na kuchangia maendeleo ya uchumi wa eneo hilo.





0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم