
Na Regina Ndumbaro
Kuna msemo unaosema "Safari ya maili elfu moja huanza kwa hatua moja." Kwa wengi, hatua hiyo huonekana ndogo na isiyo na matumaini. Lakini kwa Jafth Handeni Mwinuka, hatua hiyo ilikuwa mtaji wa shilingi laki tatu na ndoto ya kujenga biashara ambayo siku moja ingeajiri vijana na kuwahudumia maelfu ya Watanzania.
Leo, jina la JEFF ELECTRONICS (China Ndogo)limekuwa miongoni mwa biashara zinazokua kwa kasi katika sekta ya vifaa vya umeme na TEHAMA nchini, likiwa na matawi katika mikoa mbalimbali ikiwemo Ruvuma (Songea), Arusha, Songwe (Tunduma), Rukwa (Sumbawanga) na Dar es Salaam (Kariakoo), huku likiwaajiri zaidi ya vijana 50.
Lakini nyuma ya mafanikio hayo kuna simulizi ya uvumilivu, kujifunza, kuanguka na kusimama tena.
Mwaka 2010, Jafth alianza biashara yake akiwa na mtaji wa shilingi laki tatu tu. Wakati huo alikuwa Mbeya, eneo la Uyole, akijishughulisha na biashara ya kukodisha CD katika maktaba (library).Ingawa biashara hiyo ilikuwa ndogo, ndani yake kulikuwa na ndoto kubwa. Hakuridhika kubaki hapo, bali aliendelea kutafuta maarifa yaliyomwandaa kwa hatua iliyofuata.
Jafth anasema mtu aliyemshawishi kuingia kwenye biashara ni mjomba wake aliyekuwa akimiliki maduka ya vifaa vya umeme maeneo ya Uyole na Soweto jijini Mbeya.
Akiwa bado mwanafunzi, kila alipokuwa likizo alitumia muda mwingi kujifunza biashara dukani kwa mjomba wake. Baadaye, kati ya mwaka 2011 hadi 2013, alipata nafasi ya kuuza katika duka hilo, jambo lililomjengea uzoefu mkubwa wa huduma kwa wateja, uuzaji na usimamizi wa biashara.
Hapo ndipo ndoto yake ya kuwa mfanyabiashara ilipoanza kupata mwelekeo. Kwa mtazamo wake, sekta ya electronics ni biashara inayobadilika sambamba na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Anakumbuka kipindi walipoanza kuuza CD, baadaye zikapoteza soko na nafasi yake ikachukuliwa na flash disk na memory card. Leo, huduma nyingi zimehamia mtandaoni.Badala ya kuona hayo kama tishio, aliona ni fursa.
"Ukifuatilia mabadiliko ya teknolojia na ukaenda nayo, biashara ya electronics haiwezi kukutupa," anasema.Mtazamo huo ndio umeifanya JEFF ELECTRONICS kuendelea kukua sambamba na mahitaji ya soko.
Hakuna mafanikio yasiyoambatana na majaribu.Kwa Jafth, mojawapo ya changamoto kubwa imekuwa baadhi ya wafanyakazi kutokuwa waaminifu, jambo linaloweza kuathiri biashara na hata kuharibu taswira ya kampuni.
Mbali na hilo, anakiri kuwa changamoto ndogo ndogo hazikosekani katika biashara, lakini amejifunza kuwa suluhisho ni kuendelea kuelimishana, kushirikiana na kujenga utamaduni wa uwajibikaji.
Katika safari yake ya biashara, Jafth aliwahi kupata hasara kubwa baada ya mzigo wa thamani kubwa kupotea ukiwa safarini kutokana na uzembe katika upokeaji na upakiaji wa mizigo.
Kwa mfanyabiashara mwingine, huenda hilo lingekuwa mwisho wa safari.
Lakini kwake lilikuwa somo
Baada ya tukio hilo alijifunza umuhimu wa kukata bima ya mizigo. Elimu hiyo ilimsaidia kuendelea na biashara akiwa na tahadhari zaidi.
Anasema kuanguka hakumaanishi mwisho wa safari, bali ni nafasi ya kujifunza namna bora ya kusonga mbele.
Jafth anaamini mafanikio hayaji kwa bahati. Anasema msingi mkubwa uliowafikisha walipo ni imani kwa Mungu, kuamini mchakato wa mafanikio na kutokata tamaa.
Kwa maneno yake
"Ninaamini ukisubutu utakuja kuzeeka, usiposubutu pia utakuja kufa vilevile. Sisi JEFF ELECTRONICS tuliamua kufia mbele. Tunazidisha mashambulizi, Mungu juu, tukikaza mbele kweupe."
Kauli hiyo imekuwa falsafa inayowaongoza katika ukuaji wa biashara yao.
JEFF ELECTRONICS ya Leo
Kutoka biashara ndogo ya mwaka 2010, leo kampuni imepanua shughuli zake katika mikoa mbalimbali nchini.
Biashara hiyo huuza vifaa mbalimbali vya electronics ikiwemo vifaa vya wiring za nyumba, televisheni, friji, freezer, blender, kettle za umeme, sound bar pamoja na vifaa vya TEHAMA kama kompyuta za mezani, laptop, simu na vifaa vyake.
Ukuaji huo umetokana na kuendelea kusikiliza mahitaji ya wateja na kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia.
Kwa Jafth, mafanikio makubwa si ukubwa wa biashara pekee. Anasema jambo analojivunia zaidi ni kuona wateja wanaridhishwa na huduma wanazopata na kuendelea kuwaamini.
Kwake, mafanikio ya kweli ni kuhakikisha mteja anapata kile anachohitaji kwa wakati, kwa ubora na kwa huduma nzuri akiongezea kuwa Serikali na taasisi mbalimbali zimekuwa sehemu ya mafanikio yao.
Kupitia mfumo wa NeST, kampuni imepata fursa ya kushiriki katika zabuni za kusambaza vifaa kwa taasisi za Serikali na binafsi.
Pia anasema viongozi wa Serikali wamekuwa karibu nao katika nyakati mbalimbali, jambo lililodhihirika hata wakati wa uzinduzi wa tawi la Songea ambapo uongozi wa Wilaya uliunga mkono na kushiriki kufanikisha tukio hilo.Anapoulizwa ni ushauri gani anawapa vijana wanaotamani kuingia kwenye biashara, Jafth hutoa jibu lisiloegemea kwenye mtaji mkubwa.
Kwake, msingi wa biashara ni uaminifu na utu.
Anasema mtu anaweza hata kuanza bila mtaji mkubwa ikiwa atajenga uaminifu kwa wanaomzunguka.
Anatoa mfano wa kijana anayechukua bidhaa kwa mkopo, anauza na kurejesha fedha kwa uaminifu huku akijenga jina lake taratibu.
Anasisitiza kuwa biashara ni mchakato."Hakuna maisha ya mkato. Kila hatua huandaa hatua nyingine."Aidha, anawataka vijana kuzingatia mambo matatu muhimu kabla ya kuanza biashara; mtaji unaolingana na biashara husika, kuchagua eneo sahihi na kujifunza lugha nzuri ya kuwahudumia wateja.
Kwa mtazamo wake, lugha nzuri ni silaha muhimu ya mfanyabiashara.
Lengo kubwa la Jafth ni kuona JEFF ELECTRONICS inakuwa na matawi katika kila mkoa wa Tanzania.
Anasema anatamani siku moja bidhaa zitoke moja kwa moja kutoka China hadi kwenye matawi ya kampuni yaliyopo katika mikoa mbalimbali bila kupitia hatua nyingi za usambazaji.Ni ndoto ambayo anaamini inaweza kutimia kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kujenga imani kwa wateja.
Urithi anaotamani kuacha zaidi ya mali na biashara, Jafth anasema urithi anaotaka kuuacha ni upendo na uaminifu.Anataka watu wakumbuke kuwa aliendesha biashara inayowathamini wafanyakazi, inayojenga mazingira ya kazi yenye furaha na inayoweka utu mbele ya kila jambo.
Kwake, biashara si sehemu ya migogoro bali ni sehemu ya kujenga mahusiano mazuri, kuheshimiana na kukua pamoja.
Safari ya Jafth Handeni Mwinuka ni ushahidi kuwa mafanikio hayaanzi na mtaji mkubwa bali huanzia kwenye maamuzi, nidhamu, uaminifu na uvumilivu.
Kutoka shilingi laki tatu mwaka 2010 hadi kuijenga JEFF ELECTRONICS kuwa biashara inayotambulika katika mikoa mbalimbali nchini, amedhihirisha kuwa ndoto zinaweza kutimia pale mtu anapoamua kujifunza, kufanya kazi kwa bidii na kutokata tamaa.Kwa vijana wanaotamani kuingia kwenye biashara, simulizi yake ni somo kwamba changamoto si mwisho wa safari. Kila kuanguka kunaweza kuwa mwanzo wa mafanikio makubwa zaidi endapo mtu ataendelea kuamini mchakato, kulinda uaminifu na kutembea hatua kwa hatua kuelekea ndoto zake.







إرسال تعليق