KILIMO CHACHANGIA ASILIMIA 26.5 YA PATO LA TAIFA, AJIRA 65.6, SERIKALI YALENGA SEKTA KUKUA HADI 10 IFIKAPO 2030

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo akiwa ndiye mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima,Wafugaji na Wavuvi (Nanenane) kanda ya Ziwa Mashariki yaliyofanyika katika Viwanja vya Maonesho Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu Agosti 8, 2026

Na Sumai Salum –Simiyu

Sekta ya Kilimo nchini inachangia asilimia 26.5 ya Pato la Taifa, huku ikiendelea kuwa mhimili muhimu wa ajira kwa wananchi kwa kutoa ajira kwa asilimia 65.6, sambamba na kuchangia asilimia 65 ya upatikanaji wa malighafi kwa viwanda na kuhakikisha upatikanaji wa chakula kwa asilimia 100 nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, Agosti 8, 2026 akiwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya sikukuu ya nanenane kwa kanda ya Ziwa Mashariki yaliyofanyika katika Viwanja vya Maonesho Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu, akieleza kuwa takwimu hizo zinaonesha umuhimu mkubwa wa sekta ya kilimo katika uchumi na maisha ya Watanzania.

Amesema pamoja na mchango huo, Serikali inaendelea kuweka mikakati ya kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi ili ziweze kutoa mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa Taifa na kuongeza thamani ya shughuli zinazofanywa na wananchi.

"Kwa sasa, sekta ya kilimo cha mazao inakua kwa asilimia 4.2, wakati sekta ya mifugo inakua kwa asilimia 5.3, huku sekta ya uvuvi ikikua kwa asilimia 6.3" ameongeza Waziri Akwilapo.

Mhe. Dkt. Akwilapo amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha sekta hizo tatu zinaongeza kasi ya ukuaji na kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2030, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji, ajira, kipato cha wananchi na mchango wa sekta hizo katika uchumi wa Taifa.

Amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kuongeza eneo linalotumika kwa shughuli za umwagiliaji, kuboresha upatikanaji wa pembejeo na huduma za ugani, kupunguza upotevu wa chakula wakati na baada ya mavuno, pamoja na kuimarisha masoko ya bidhaa za kilimo, mifugo na uvuvi.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kuimarisha tafiti na matumizi ya teknolojia za kisasa katika sekta hizo ili kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao, mifugo na bidhaa za uvuvi, huku matumizi bora ya ardhi yakipewa kipaumbele katika kufanikisha malengo hayo.

Katika hatua nyingine, Dkt. Akwilapo amesema Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ipo tayari kushirikiana na mikoa inayounda Kanda ya Ziwa Mashariki pamoja na Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kuboresha Viwanja vya Maonesho Nyakabindi ili viwe vya kisasa na viendane na mahitaji ya shughuli zinazofanyika katika eneo hilo.

Amesema Wizara itashirikiana na wadau hao kuandaa ramani na mpangilio wa eneo la viwanja kulingana na mahitaji, hatua iliyokuja baada ya ombi lililowasilishwa kupitia taarifa iliyosomwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anamringi Macha, wakati wa kilele cha maadhimisho hayo.

Dkt. Akwilapo amesema maboresho hayo yatawezesha viwanja hivyo kuwa na mazingira bora na ya kisasa kwa ajili ya maonesho na shughuli mbalimbali za sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, sambamba na kusaidia wananchi kujifunza teknolojia na fursa zinazopatikana katika sekta hizo.

Ameongeza kuwa Serikali inalenga kuhakikisha Tanzania inafikia uchumi wa kati wa juu ifikapo mwaka 2050, kutoka uchumi wa kati wa chini ambao nchi iliingia mwaka 2021, akisisitiza kuwa mafanikio hayo yatategemea kwa kiasi kikubwa uwezo wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kuongeza ushirikishaji, uzalishaji na kufikia malengo yaliyowekwa.

Kwa ujumla, Serikali inaeleza kuwa matumizi bora ya ardhi, upanuzi wa umwagiliaji, upatikanaji wa pembejeo, masoko, tafiti na teknolojia ni miongoni mwa nguzo muhimu zitakazosaidia Tanzania kufikia malengo yake ya maendeleo kuelekea mwaka 2050. 
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anamringi Macha akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima,Wafugaji na Wavuvi (Nanenane) kanda ya Ziwa Mashariki yaliyofanyika katika Viwanja vya Maonesho Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu Agosti 8, 2026
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe Mboni Mhita akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima,Wafugaji na Wavuvi (Nanenane) kanda ya Ziwa Mashariki yaliyofanyika katika Viwanja vya Maonesho Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu Agosti 8, 2026
Katibu Tawala mkoani Shinyanga CP. Salum Hamdun akifuatilia kwa makini kilele cha maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima,Wafugaji na Wavuvi (Nanenane) kanda ya Ziwa Mashariki yaliyofanyika katika Viwanja vya Maonesho Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu Agosti 8, 2026
Katibu Tawala wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Fatma Mohamed 
Katibu Tawala wilayani Kahama Mkoani Shinyanga  Glory Absalum
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga Khadija kabojela 


















































































0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم