Na WMA - Dodoma
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Bw. Alban Kihulla, amekutana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Bw. Salum Mnuna, jijini Dodoma tarehe 17 Agosti 2026, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya taasisi hizo mbili katika sekta za mafuta, gesi, maji na umeme.
Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano na uratibu wa kiutendaji, kubadilishana taarifa za kimkakati, pamoja na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo mbili katika sekta za mafuta, gesi, maji na umeme, kwa lengo la kuimarisha usimamizi, kulinda maslahi ya walaji na kuhakikisha utoaji wa huduma wenye tija na unaozingatia haki.
Viongozi hao walisisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa vifaa vyote vya kupimia vinavyotumika katika utoaji wa huduma na biashara vinatoa vipimo sahihi na vinavyoaminika, hatua ambayo ni muhimu katika kulinda maslahi ya walaji, wafanyabiashara na watoa huduma.
WMA, ikiwa na jukumu la kuhakikisha usahihi wa vipimo vinavyotumika katika biashara, itaendelea kushirikiana kwa karibu na EWURA ili kuimarisha haki katika miamala, uwazi, uwajibikaji na thamani ya fedha kwa mlaji.
Ushirikiano huo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kujenga mazingira ya biashara yenye haki na kuimarisha imani ya wananchi katika mifumo ya vipimo na huduma zinazotolewa nchini.
“Vipimo Sahihi, Haki ya Mlaji.”


إرسال تعليق