DIWANI MAGANZO ATOA "PRINTER" NA KOMPYUTA KUSAIDIA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU SHULENI

Diwani wa Kata ya Maganzo, Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Hamza Tandiko akizungumza kwenye mahafali ya dalasa la saba Shule ya msingi Maganzo wilayani Kishapu Septemba 30,2026


Diwani wa Kata ya Maganzo, Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Hamza Tandiko, ameshiriki katika hafla ya kuwaaga wahitimu wa Elimu ya Msingi ya Shule ya Msingi Maganzo kwa mwaka 2026, iliyowakutanisha wazazi, walezi na walimu, huku akitoa mashine moja ya kuchapisha (printer) kwa ajili ya kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya walimu shuleni hapo.


Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika Septemba 30, 2026, Mhe. Tandiko amesema lengo la kutoa printa hiyo ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu, pamoja na kusaidia walimu kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.


Amesema akiwa Diwani wa Kata ya Maganzo, ana wajibu wa kushirikiana na jamii pamoja na taasisi mbalimbali katika kutafuta na kusaidia upatikanaji wa mahitaji muhimu yanayoweza kuchangia maendeleo ya kata, hususan katika sekta ya elimu.


Mhe. Tandiko amesema printer hiyo ni sehemu ya jumla ya printer mbili ambazo ametoa katika shule za msingi ndani ya Kata ya Maganzo, ambapo moja imetolewa katika Shule ya Msingi Maganzo na nyingine katika Shule ya Msingi Masagara, ikiwa ni hatua ya kuendelea kusaidia walimu katika utekelezaji wa majukumu yao.


Aidha, amesema juhudi hizo hazitaishia hapo, kwani anatarajia kutoa kompyuta mbili kati ya nne ambazo zimeombwa na Shule ya Sekondari Maganzo, ili kusaidia shule hiyo katika kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji pamoja na matumizi ya teknolojia katika elimu.


Amesema mpango huo ni mwendelezo wa jitihada alizoanza katika Shule ya Sekondari Masagara, ambako amewahi kutoa kompyuta pamoja na baadhi ya samani za ofisi, huku pia Shule ya Msingi Masagara ikipewa printer.


Mhe. Tandiko amesema hatua hizo zinaendana na dhamira yake ya kuhakikisha elimu katika Kata ya Maganzo inatolewa kwa ufanisi, akisisitiza kuwa kauli yake ya "kusema na kutenda” itaendelea kuonekana kupitia vitendo vinavyolenga kuboresha huduma kwa wananchi, hususan katika sekta ya elimu.


Pamoja na hayo, amewapongeza walimu wa Kata ya Maganzo kwa kazi wanayoifanya na kuwataka kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, weledi na kuzingatia viapo vyao vya utumishi, huku wakimtanguliza Mungu katika utekelezaji wa majukumu yao.


Aidha, Mhe. Tandiko ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mkazo katika upatikanaji wa elimu bila malipo na kuhakikisha watoto wanapata fursa ya kupata elimu.


Kwa upande wa wazazi na walezi, ametoa rai ya kuendelea kushirikiana kwa karibu na walimu katika kuhakikisha watoto wanahudhuria shule kwa wakati na kupunguza utoro, huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha wanafunzi wanapata lishe bora ili waweze kujifunza katika mazingira mazuri.


Amesema mafanikio ya elimu yanahitaji ushirikiano wa walimu, wazazi, walezi, viongozi na jamii kwa ujumla, hivyo kila mmoja anapaswa kutekeleza wajibu wake katika kuhakikisha watoto wanapata elimu bora na malezi yanayowajenga kuwa raia wema wa taifa.


 Tandiko anaendelea kuonesha mfano wa uongozi unaokwenda sambamba na vitendo, akitumia nafasi yake kama Diwani wa Kata ya Maganzo kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali katika kutatua changamoto na kuimarisha huduma za kijamii, hususan elimu. Juhudi hizo zinaendelea kuwa chachu ya kuwahamasisha viongozi wengine kuweka nguvu katika vitendo vinavyogusa maisha ya wananchi na kuchangia maendeleo ya Kata ya Maganzo.

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم